1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mateka zaidi wa Israel waachiwa na Hamas

30 Novemba 2023

Katika siku ya mwisho ya muda wa nyongeza wa usitishwaji mapigano kati ya Israel na Hamas, jeshi la Israel IDF limesema mateka 14 zaidi 10 kati yao wakiwa Waisraeli, wamekabidhiwa Shirika la Msalaba Mwekundu.

https://p.dw.com/p/4ZbOW
Israel Hamas Mateka | Kivuko cha mpakani cha Rafah
Gari la Shirika la Msalaba Mwekunde lililowabeba mateka walioachiwa na HamasPicha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Jeshi hilo na Hamas, wote wamethibitisha kwamba watu hao ni Waisraeli na raia 4 wa Thailand.

Wakati huo huo, jeshi la Israel limeandika kwenye mtandao wa kijamii kwamba mateka wengine wawili wa Israeli wamekabidhiwa maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu na kwa sasa wako njiani kuelekea Israel. Watu hao wanadaiwa kuwa raia wa Urusi pia.

Kundi la Hamas ambalo linaorodheshwa kama kundi la kigaidi na Marekani, Umoja wa Ulaya, Ujerumani na nchi nyengine, mapema lilisema kwamba wanawake hao wawili waliachiwa "baada ya juhudi za rais wa Urusi."

Katika siku kadhaa zilizopita, watu walio na uraia wa nchi mbili au raia wa kigeni wamekuwa wakiachiwa kama nyongeza ya ubadilishanaji wa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas na wafungwa wa Palestina.

Jeshi la Israel lawauwa Wapalestina 3

Mbali na hayo jeshi la Israel limesema limewauwa Wapalestina watatu waliokuwa wamejihami katika Ukanda wa Gaza jana Jumatano, licha ya usitishwaji wa mapigano uliokubaliwa. Haya yamesemwa na msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari ambaye hakutoa taarifa zaidi.

Wakimbizi wakimbia jeshi la Israel: Wapalestina waelekea kusini na kati mwa Ukanda wa Gaza
Wapalestina wakikimbia Gaza kaskaziniPicha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Vyanzo vya kimatibabu katika Ukanda wa Gaza vimesema watu wawili waliouwawa na mtu mmoja aliyejeruhiwa wamepatikana katika eneo la kaskazini la ukanda huo. Kulingana na mashuhuda, watu hao walikuwa hawakujihami ingawa taarifa hiyo haikuweza kuthibitishwa kwa njia huru.

Kulikuwa na ufyatulianaji risasi hapo Jumanne usiku kaskazini mwa Ukanda wa Gaza huku pande zote zikilaumiana kwa ukiukaji wa muda wa usitishwaji mapigano. Muda huo wa kusitishwa mapigano ulioanza Ijumaa iliyopita, unaweza kudumu hadi asubuhi ya leo, ingawa majadiliano yanayosimamiwa na Qatar na Misri yanaendelea kutazama iwapo muda huo utaongezwa.

Kwengineko China ambayo inashikilia urais wa muda wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, imeitisha mkutano jana Jumatano, ambapo waziri wake wa mambo ya nje Wang Yi ameliambia baraza hilo kwamba, mzozo unaoendelea sasa unaonyesha haja ya suluhisho la mataifa mawili ili amani ya kudumu iweze kupatikana.

Kama alivyosema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa awali katika hotuba yake kwenye baraza hilo, Yi amesema kuna haja ya dharura ya mapigano kusitishwa kwa muda mrefu.

Wakati huo huo, balozi wa Israel wa Umoja wa Mataifa Gilad Erdan amekiambia kikao cha Baraza la Usalama kwamba kuunga mkono usitishwaji wa kudumu wa mapigano ni sawa na kuliunga mkono kundi la Hamas kuendelea kuudhibiti Ukanda wa Gaza, jambo ambalo kundi hilo la wanamgambo limefanya tangu mwaka 2007.

Naye balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield amesema huku Israel ikiendelea "kutumiza haki yake ya kuwalinda watu wake kutokana na vitendo vya kigaidi" Marekani imeitaka ichukue hatua zozote kuzuia au kupunguza mauaji ya raia.

Miundombinu ya hospitali Gaza inastahili kulindwa

Hayo yakiarifiwa, msemaji wa jeshi la Israel IDF, Kanali Peter Lerner,ameiambia DW kuwa upo uwezekano kwamba jeshi la Israel linaweza kupanua operesheni yake kusini mwa Gaza. Lerner amesema kwa sasa jeshi la Israel linaendelea kushikilia nafasi za kujilinda kaskazini mwa Gaza na kuandaa mipango yao ya hatua inayofuata ya mashambulizi.

Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu awatembelea wanajeshi Ukanda wa Gaza
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akikutana na wanajeshi wa Israel Ukanda wa GazaPicha: Avi Ohayon/GPO/Handout via REUTERS

Msemaji huyo wa jeshi vile vile amesema kuwa operesheni ya jeshi kaskazini mwa Gaza haijakwisha na kwamba watavipeleka vita mlangoni mwa Hamas popote pale wanapojificha kwa ajili ya kulifikia lengo lao la kulisambaratisha kundi hilo ambalo kulingana na Lerner, linawashikilia mateka Waisraeli, raia wa kigeni na hata watu wa Gaza.

Hayo yakijiri, mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, ametoa wito wa juhudi za kuilinda miundombinu ya hospitali Gaza iliyo katika hali mbaya. Ghebreyesus amesema ni hospitali 15 tu kati ya 36 zilizoko Gaza, ambazo zinafanya kazi na kwa sasa zimelemewa kabisa.

Shirika hilo la afya ulimwenguni pia limeonya kuhusiana na hatari ya magonjwa ya kuambukiza kuenea katika hospitali hizo ambazo hazina vifaa na madawa ya kutosha.

Vyanzo: DPA/AP/DW /dw/en/israel-hamas-war-more-hostages-handed-over-to-the-red-cross/live-67579411