Matokeo ya uchaguzi wa bunge nchini Israel
23 Januari 2013Waisraeli wamepiga kura jana, na wamezusha maajabu. Mtangazaji wa zamani wa televisheni, Jair Lapid na chama chake cha kiliberali - Yesh Atid - amemaliza nafasi ya pili akijikingia viti 19 vya bunge la Knesset. Yeye ndiye mshindi mkubwa wa uchaguzi huo. Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameondolewa patupu na wapiga kura. Muungano wa vyama vya mrengo wa kulia vya Likud na Beitenu, anaouongoza, umejipatia viti 31 toka jumla ya viti 120 vya bunge la Israel - Knesset.
Baada ya ushindi kama huo, kimsingi mshindi hupanda ndani ya gari la fakhari. Yair Lapid lakini hakutaka makubwa na badala yake ameamua kupanda teksi kutoka nyumbani kwake kwenda katika ukumbi wa sherehe zilizoandaliwa na chama chake.Mshindi halisi wa uchaguzi huo Yair Lapid anasema:"Taifa la Israel linakabiliwa na changamoto kubwa. Inabanwa na mgogoro wa kiuchumi ambao ni kitisho kwa watu wa tabaka la wastani. Israel inakumbwa na kitisho cha kutengwa kimataifa. Njia ni moja tu kuweza kuzishinda changamoto hizo; Ushirikiano na mshikamano."
Uchaguzi ni fursa ya mageuzi
Ilikuwa zaidi ya saa sita unusu za usiku pale mwanasiasa huyo mpya alipojiunga na waafuasi wa chama chake cha "Yesh Atid" kusherehekea ushindi wa viti 19 kati ya 120 vya bunge la Israel, Knesset. Na takriban wakati huo huo, waziri mkuu Benjamin Netanyahu alikamata kipaza sauti kuwahutubia wafuasi wake. Vituo vya televisheni vya Israel vilipata shida kuwaonyesha wote wawili kwa wakati mmoja.
Katika matangazo ya moja kwa moja, vituo vya televisheni vilibakia kumuonyesha kwanza mshindi akihutubia na baadaye aliyeshindwa. Mwanasiasa aliyeshindwa ambaye pengine ataendelea kuwa waziri mkuu, Benjamin Netanyahu, amejiwekea malengo matano abayo ni:"Kuizuia Iran isimiliki silaha za kinyuklia, kutuliza uchumi wa Israel, jitihada za amani pamoja na wapalestina, jukumu la kulitumikia jeshi hata miongoni mwa wanafunzi wa kiorthodox na kupunguza matumizi."
Netanyahu anataka kuunda serikali pana ya muungano. Tokea hapo hana njia nyengine. Na anajipiga kifua anapojidai matokeo ya uchaguzi ni fursa ya kutekeleza mageuzi wanayoyataka Waisraeli. Lakini kwa waziri mkuu aliyeadhibiwa vibaya sana na wapiga kura, haitakuwa kazi rahisi kuunda serikali ya muungano. Netanyahu atakumbana na mwanasiasa mwengine mpya, Naftali Benett, anayekiongoza chama cha kihafidhina cha Habait Hajehudi, anayepigania zaidi kuendelezwa ujenzi wa makaazi ya wahamiaji wa kiyahudi.
Nafasi ya vyama vya mrego wa shoto
Lakini pia kuna wanasiasa wanaotarajia matokeo ya uchaguzi yataleta mageuzi ya kweli. Mkuu wa chama cha Labour, Shelly Yachimovich, anasema wanabidi wasubiri matokeo ya mwisho rasmi ya uchaguzi. Mbali na chama cha Labour, chama cha waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje, Tzipi Livni, nacho pia kimefanikiwa kuwakilishwa bungeni.
Mwandishi: Wagner Christian/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Josephjat Charo