1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Masoko ya Hisa yaashiria Mema

22 Juni 2015

Thamani katika masoko ya hisa barani Ulaya na nje ya kanda ya Euro zimepanda kufuatia wimbi la matumaini pengine Ugiriki na wafadhili wa kimataifa wakafikia makubaliano yatakayoiepushia Ugiriki balaa la kufilisika.

https://p.dw.com/p/1FkgO
Maandamano ya mshikamano pamoja na Ugiriki mjini BrusselsPicha: picture-alliance/dpa/V. Mayo

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras atakutana na viongozi wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya,benki kuu ya Ulaya na shirika la fedha la kimataifa kabla ya mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro utakaoitishwa usiku kwa lengo la kusaka makubaliano kuhusu mzozo wa madeni ya Ugiriki.

Safari ya waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras mjini Brussels leo hii imefuatia mashauriano ya nguvu hapo jana pamoja na baadhi ya wafadhili muhimu akiwemo kansela Angela Merkel wa Ujerumani,rais Francois Hollande wa Ufaransa na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Juncker-wote wakipania kuiona Ugiriki inasalia mwanachama wa kanda ya Euro na kwa namna hiyo kuepukana na kizungumkuti .

Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker ameyataja mapendekezo mepya ya Ugiriki "kuwa msingi mzuri wa kufikia maendeleo" huku kamishna wa Umoja wa ulaya anaeshughulikia masuala ya kiuchumi,Pierre Moscovici akisema "anaamini makubaliano yatapatikana."

Masoko ya hisa yapalilia matumaini

Masoko ya hisa yanaonyesha kuwapa moyo wahusika wa kasheshe ya madeni ya Ugiriki.Masoko ya hisa ya Ujerumani yamepanda kwa asili mia mbili nukta tano na dhamana za mikopo za Uhispania na Italy zimeporomoka kwa pointi 12.Dax la Ujerumani limepanda kwa asili mia 3,CAC 40 ya Ufaransa kwa asili mia 2.5 na FTSE la Uengereza kwa asili mia 1.5.

Symbolbild Börse in Frankfurt am Main
Soko la hisa la Ujerumani mjini FrankfurtPicha: picture-alliance/dpa/F. Rumpenhorst

"Kuna uwezekano mkubwa,makubaliano yatafikiwa" amesema mtaalam mmoja wa benki mashuhuri ya Uswisi-Credit Suisse.

Mapendekezo hayo mepya ya Ugiriki ndiyo yatakayojadiliwa katika mkutano wa kilele wa viongozi wa19 wa kanda ya Euro leo usiku mjini Brussels.Wengi wa wakaazi wa Ugiriki wanayawekea matumaini mazungumzo hayo:

"Tunasubiri makubaliano lakini pia tunahofia hatua mpya.Nataraji safari hii watatuhurumia.Ni shida kidogo,lakini tutayajua leo usiku."Anasema mkaazi mmoja wa Athens.

Wakaazi wa Ugiriki wasubiri

Nchini Ugiriki kwenyewe matumaini ya kufikiwa makubaliano pamoja na wafadhili yamepelekea masoko ya hisa nchini humo pia kupanda.Ugiriki inahitaji Euro bilioni moja nukta tano hadi juni 30 ijayo kuweza kulilipa shirika la fedha la kimataifa IMF na kwa namna hiyo kuepukana na balaa la kufilisika.

Griechenland legt neuen Vorschlag vor Alexis Tsipras ARCHIV
Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis TsiprasPicha: Reuters/P. Hanna

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman