1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huenda Ugiriki ikapata nafuu juu ya deni lake

Mjahida 10 Julai 2015

Waziri wa Uchumi wa Ufaransa ameelezea matumaini kuhusu kupatikana makubaliano baina ya Ugiriki na mataifa mengine ya Ukanda wa Euro, akisema taifa hilo limepiga hatua kubwa katika mapendekezo yake ya hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/1FwG1
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras na wanasiasa wenzake
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras na wanasiasa wenzakePicha: Reuters/J.-P. Pelissier

Siku moja tu baada ya Ugiriki kuwasilisha mapendekezo yake kuhusu mageuzi hayo, waziri huyo wa Uchumi wa Ugiriki, Emmanuel Macron amesema kiwango cha mageuzi hayo kinaendana na kile kinachotarajiwa na kuongeza kuwa hatua hiyo inatoa matumaini ya makubaliano kuafikiwa.

"Yapo mageuzi kadhaa yaliyo wazi ambayo yamependekezwa na serikali ya Ugiriki ambayo yanatufanya tuamini kwamba kiwango cha mageuzi yenyewe kinaweza kutimiza malengo yaliyotarajiwa," alisema Macron alipokuwa katika kongamano wakati wa ziara yake ya Madrid

Naye Rais wa Ufaransa, Francois Hollande amesema leo hii kuwa mapendekezo ya hivi punde ya Ugiriki kuhusu mpango wa mageuzi yatakayoliwezesha taifa hilo kupewa mikopo, yana uzito na yenye kuaminika. Ameongeza kuwa:

Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis TsiprasPicha: picture-alliance/dpa/P. Seeger

"Saa zinazokuja zitakuwa muhimu. Hakuna uamuzi uliofanywa hadi sasa kwa vile maafisa wa mataifa ya ukanda wa euro watatathmini yaliyomo siku ya Jumapili kabla ya kuyawasilisha mbele ya viongozi wa Umoja wa Ulaya siku itakayofuata."

Ufaransa yashinikiza kupatikana kwa makubaliano

Ikumbukwe kwamba Ufaransa, miongoni mwa mataifa yenye ushawishi mkubwa miongoni mwa yale ya ukanda wa euro imekuwa ikishinikiza kupatikana kwa makubaliano ili Ugiriki iendelee kusalia katika ukanda huo wa ero.

Wakati uo huo, Soko la Hisa la Ulaya limeyaunga mkono mapendekezo ambayo serikali ya Ugirki iliwasilisha kwa wakopeshaji wake ambao Shirika la Fedha la Kimataifa IFM, Umoja wa Ulaya na Benki Kuu ya Ulaya.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande
Rais wa Ufaransa Francois HollandePicha: Reuters/E. Vidal

Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras aliwasilisha stakabadhi yenye maelezo kuhusu mageuzi hayo kwa wakopeshaji wake muda mfupi kabla ya Alhamisi usiku wa manane kwa lengo la kulinururu taifa hilo dhidi ya kuporomoka kiuchumi. Miongoni mwa mapendekezo hao ni mpango wa kuongeza viwango vya kodi na megeuzi mengine kuhusu malipo ya uzeeni.

"Tunayo matumaini, tuna matumaini ya maelewano mazuri, tuna matumaini," alisema Waziri wa Ndani wa Ugiriki Nikos Voutsis.

Bunge la Ugiriki leo hii litapiga kura kuhusu mapendekeo hayo ya mageuzi huku uungwaji mkono wa wakopeshaji wa nchi hiyo ukisalia kuwa jambo muhimu ili viongozi wa ukanda wa uero waidhinisha mpango huo kwenye mkutano utakaofanyika Jumapili.

Mwandishi: Geoffery Mung'ou/AFP/Reuters

Mhariri: Mohamed Abdul'Rahman