Mauaji ya Orlando yalaaniwa
13 Juni 2016Tukio la shambulizi hilo ambalo linaelelezwa kuwa baya zaidi katika historia ya hivi karibuni nchini humo lililofanyika jumapili tarehe 12.06.2016 lilipelekea polisi katika mji wa Orlando kuingia katika eneo hilo la tukio na kumua mshambuliaji huyo kwa kumpiga risasi.
Mauaji hayo yameibua majonzi katika jamii ya mashoga nchini humo na kuwalazimu mashoga zaidi ya 100 kuandamana mjini Los Angeles kulaani tukio hilo.
Mjini New York tuzo za maalumu za muziki almaarufu Tony Awards ziliendelea kufanyika kama zilivyokuwa zimepangwa lakini pia zikibeba ujumbe wa kuwaenzi wahanga wa mashambulizi hayo.
Rais Obama alaani mauaji hayo
Rais wa Marekani Barack Obama amelaani mauaaji hayo na kulifananisha shambulizi hilo na tukio la kigaidi na chuki.
Amesema kama wamarekani wanaungana kwa pamoja kuomboleza vifo hivyo na pia kuwalinda watu wao.
Watu mashuhuri kutoka miongoni mwa jamii ya kiisilamu nchini Marekani pamoja na kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis na pia viongozi wengine wa kidunia wamelaani shambulizi hilo ambalo linaonekana kuwa shambulizi moja baya zaidi kufanyika katika ardhi ya Marekani tangu yale mashambulizi ya Septemba 11, 2001 nchini humo.
Shirika la ujasusi la Marekani lilikiri kuwa mtu anayedaiwa kufanya shambulizi hilo Omar Mateen mwenye umri wa mika 29 awali alikuwa amekwisha fanyiwa uchunguzi na kubainika kuwa hakuwa na mahusiano na makundi ya kigaidi.
Hata hivyo taarifa zaidi za kiintelejensia zilizofanywa na wakala maalumu aitwaye Ronald Hopper zilibaini kuwa Mateen alikuwa tayari amefanya mawasiliano kwa njia ya simu yaliyoonyesha utiifu wake kwa kundi la itikadi kali la Dola la Kiisilamu la IS muda mchache kabla ya kufanyika mauaji hayo.
Wito watolewa kutohusisha uisilamu na shambulizi hilo
Kwa upande wake Kyle Brown mwenye umri wa miaka 21 ambaye alikuwa miongoni mwa vijana wengi waliojitokeza katika mitaa ya mji wa Orlando jumapili usiku kuonyesha hisia zao za kulaani mauaji hayo akizungumza na shirika la habari la dpa alipuuza hoja ya watu wanaohusisha shambulizi hilo na jamii ya kiisilamu kwa sababu tu ya tukio lililofanywa na mtu mmoja.
Wakati huohuo shirika moja la habari lenye mahusiano na kundi la itikadi kali la IS la Amaq limetoa kauli pasipo kutoa ushahidi kuwa mmoja wa wapiganaji wake alihusika na shambulizi hilo.
Mateen alizaliwa na wazazi wenye asili ya Afghanistan mjini New York mnamo mwaka 1986 na kuishi katika kitongoji cha Port St Lucie, katika jimbo la Florida ambapo ni mwendo wa karibu saa mbili kutoka mji wa Orlando.
Mwandishi : Isaac Gamba /afpe/dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga