1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri kujadili mkataba wa kulinda Bioanuai mjini Montreal

15 Desemba 2022

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Bioanuai unaingia hatua muhimu wakati mawaziri wa mazingira wakiwasili Montreal kutafuta makubaliano ya mwisho ya kupunguza kitisho cha kutoweka kwa viumbehai na makaazi yao duniani.

https://p.dw.com/p/4L08K
UN-Artenschutzkonferenz COP 15 in Montreal, Kanada 2022 | Themenbild
Picha: Christina Muschi/REUTERS

Mazungumzo hayo ya hatua ya mwisho yatakayowajumuisha mawaziri wa mazingira kutoka karibu nchi 196 duniani yanabeba matumaini ya kufikiwa kile wanaharakati wa mazingira wanakiita kuwa "mkataba wa amani na mazingira yetu”.

Majadiliano yanatarajiwa kuwa magumu juu ya nani anafaa kubeba dhima kubwa zaidi katika kulinda bioanuai na hatari ya kutoweka kwa jamii chungunzima za mimea na spishi za wadudu na wanyama kwenye uso wa dunia.

Tangu kuanza mkutano huo wiki iliyopita migawanyiko bado ni mikubwa na hakuna dalili za kupatikana mwafaka.

Suala tete kama ilivyokuwa kwenye mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa COP27 uliomalizika hivi karibuni nchini Misri, ni fedha na vipi zitapatikana.

Njia za kukusanya fedha na kiwango cha mchango bado ni kizingiti

UN-Artenschutzkonferenz COP 15 in Montreal, Kanada 2022 | Themenbild
Picha: Andrej Ivanov/AFP/Getty Images

Wawakilishi wa mkutano huo wa Montreal wanajadili ni kiasi gani cha fedha ambacho nchi tajiri zinapaswa kuzitoa kuyasaidia mataifa masikini kulinda mifumo ya Ikolojia.

Kuna pendekezo pia la kuundwa fuko maalumu la michango ya kifedha kusaidia shughuli hizo. Lakini yote hayo bado hayajaafikiwa na mawaziri wa mazingira watajaribu kushinikiza kupatikana makubaliano.

Kilicho rehani ni hatma ya sayari ya dunia na iwapo binadamu watakuwa tayari kupunguza uharibifu wa makaazi ya viumbehai wengine kupitia uchafuzi wa mazingira na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi.

Wataalamu wa sayansi wanasema, matatizo yote hayo yanatishia kuangamiza mamilioni ya spishi za viumbe vya nchi kavu na baharini.

Rasimu ya mkataba unaotafutwa inajumuisha zaidi ya malengo 20, ikiwemo ahadi kubwa kabisa ya kuhifadhi asilimia 30 ya eneo la ardhi na bahari duniani ifikapo mwaka 2030.

Mengineyo ni kuzuia uvumi haramu, kupambana na jamii za spichi vamizi mfano wa magugu na kupunguza matumizi ya dawa za kuua wadudu zinazoaminika kuwa chanzo cha kuharibu mazalia ya wadudu muhimu kama nyuki.

Makubaliano yanaweza kupatikana lakini kwa mbinde

UN-Artenschutzkonferenz COP 15 in Montreal, Kanada 2022 | Protest in PARIS, Frankreich | Extinction Rebellion
Wanaharakati wa mazingira wakiandamana kuonesha athari za uharibifu wa mazingira kwa Bioanuai.Picha: Anna Kurth/AFP/Getty Images

Majadiliano ya awali kwenye mkutano huo tayari yamesadifu kuwa magumu. Mnamo siku ya Jumanne wawakilishi wa mataifa masikini walitoka nje ya ukumbi baada ya kushindwa kuafikiana na wenzao kutoka mataifa tajiri juu ya ni vipi fedha za kufanikisha miradi ya kulinda Bioanuai zitapatikana.

Mataifa masikini ambayo ndiyo yenye hifadhi kubwa ya misitu na makaazi ya viumbe hai yanataka liundwe fuko la fedha la kupiga jeki miradi ya bioanuai lakini nchi tajiri zinapinga pendekezo hilo.

Hoja ya nchi masikini ni kwamba mfumo wa sasa wa utoaji fedha kama hisani hautoshi kufikia malengo ya kunusuru viumbehai.

Mataifa mfano wa Brazil, Indonesia na mengine kadhaa ya Afrika, yanataka alau dola bilioni 100 zipatikane kila mwaka hadi ifikapo 2030 kufanikisha ajenda ya uhifadhi duniani.

Na pendekezo hilo kwa hakika linaonesha kuwa mfupa mgumu kwenye mazungmzo ya mjini Montreal.