Mawaziri wa ASEAN wasisitiza ushirikiano zaidi
31 Julai 2019Mkutano huo umeghubikwa na ongezeko la mzozo wa kiusalama kwenye rasi ya Korea, madai ya kibabe ya China juu ya umiliki wa maeneo ya bahari ya China Kusini pamoja na vita vya kibiashara kati ya Marekani na China.
Ikitafuta kuimarisha sauti yake kama mdau muhimu katika masuala ya kidunia, Jumuiya ya ASEAN pia imewakaribisha mawaziri kadhaa wa mambo ya nje kutoka mataifa muhimu washirika na washirika wa majadiliano, akiwemo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, waziri Mkuu wa Thailand na mwenyekiti wa jumuiya ya ASEAn kwa mwaka huu wa 2019, Prayuth Chan-ocha, aliwataka mawaziri hao kubuni mkakati wa pamoja kusonga mbele, kubuni ushirika thabiti na "marafiki zetu kote duniani, mashirika ya kimataifa na sekta zote za jamii."
Wito wa kutazama mbali zaidi
Mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu, waziri wa mambo ya nje wa Thailand Don Pramudwinai, aliwaambia wenzake katika jumuiya hiyo inayoundwa na mataifa 10 ya kusini mwa Asia kwamba wanapaswa kuwa wepesi zaidi katika wakati huu ambapo hisia za uzalendo zinaongezeka duniani.
"Viongozi wetu wamezungumzia haja kwa ASEAN kuwa na mtazamo mpana zaidi na kuimarisha umoja ili kuzungumza kwa sauti moja ili tuweze kusikika. Pia tumeridhia waraka muhimu kuhusu mtazamo wa ASEAN juu ya kanda ya bahari ya Hindi na Pasifiki ambao unatoa muongozo wa ushirikiano wa kivitendo na mataifa yaliomo kwenye kanda hiyo."
Ameonya kuwa safari iliyoko mbele yao inaweza kuwa ngumu lakini akasema ushirikiano zaidi miongoni mwa mataifa wanachama wa ASEAN na washirika wa nje unaweza kusaidia kuendeleza ukuaji wa muda mrefu.
Mapambano ya kuwania ushawishi kati ya Marekani na China yameiweka kanda ya ASEAN katika wakati mgumu. Viongozi wa kanda hiyo katika mkutano wao wa kilele mwezi Juni waliridhia mkakati huo wa ushirikiano kati yao na mataifa ya Bahari za Hindi na Pasifiki, na pia waliazimia kuwa na ushirikiano mwema na Marekani na China.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,rtrtv
Mhariri: Sekione Kitojo