Tunaunga mkono mazungumzo zaidi kuhusu Urusi-Borrell
21 Februari 2022Mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi za Umoja wa Ulaya wanakutana Brussels kulijadili suala la mgogoro kuhusu Ukraine miongoni mwa mengine. Na tayari mkuu wa sera za nje wa Umoja huo Joseph Borrell ameshasema kwamba Umoja huo hautoiwekea vikwazo Urusi kwa sasa, tamko ambalo linaonesha kuupinga mwito unaotolewa na Kiev wa kuitaka jumuiya hiyo ichukue hatua hizo ili kuepesha vita.
Kabla ya mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya kuanza mjini Brussels,mkuu wa sera za nje wa Jumuiya hiyo Joseph Borrell ameweka wazi kwamba bado Umoja huo hautoiwekea vikwazo Urusi,ingawa Ukraine inasisitiza Jumuiya hiyo inapaswa kuchukua hatua hizo kuliko kusubiri mpaka Urusi itakapofanya uvamizi.
Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba,baada ya kuwasili kushiriki mkutano wa Brussels amesema wanataraji kuona maamuzi ya dhidi ya Urusi yanafanyika.
''Maamuzi ambayo Umoja wa Ulaya inaweza kuyafanya kutuma ujumbe wa wazi kwa Urusi kwamba uchokozi wake hauwezi kukubalika na Ukraine haitokuwa peke yake,sio tu ni ya kisiasa bali pia ni pamoja na kuchukuliwa hatua kadhaa mahususi kama vile kuunga mkono juhudi zetu katika sekta ya ulinzi,kusaidia usalama wa kimtandao na kupitisha baadhi ya vikwazo.Na huu ndio ujumbe ntakaowafikishia wenzangu katika mkutano wa leo.''
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ukraine ameendelea kusema kwamba wanaamini kuna sababu za kutosha na za halali za kuiwekea vikwazo Urusi hivi sasa ili kuonesha,Umoja wa Ulaya sio tu unapiga kelele kuhusu vikwazo lakini pia unachukua hatua za kutekeleza kwa vitendo.
Waziri Kuleba atahutubia mkutano huo wa kilele wa kawaida wa kila mwaka mjini Brussels wa mawaziri wa mambo ya nje. Lakini mkuu wa sera za nje wa Umoja huo Joseph Borrell pamoja na baadhi ya mawaziri kutoka nchi kadhaa wameshasema waziwazi kwamba jumuiya hiyo haina mpango hivi sasa wa kuiwekea Urusi Vikwazo ingawa pia Borrell amesema ataitisha mkutano maalum wa Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kukubaliano vikwazo pale muda utakapofika.
Kwa mujibu wa Borrell Umoja wa Ulaya hivi sasa unaunga mkono juhudi zaidi za mazungumzo.
Kwa upande mwingine waziri wa mambo ya nje wa Lithuania Garielius Landsbergis, ameuambia Umoja wa Ulaya lazima uweke vikwazo vya ziada dhidi ya Belarus kutokana na hatua ya nchi hiyo kuwapokea wanajeshi wa Urusi.
Mkutano wa Brussels wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya pia umejadili kuhusu mgogoro wa Bosnia,Mawaziri wakitafuta njia za kuondowa migawanyiko Bosnia ili kuepusha uwezekano wa kugawika mapande mawili taifa hilo la Balkan katika wakati ambapo makubaliano ya amani ya Bosnia Harzegovina yaliyofikiwa zaidi ya miaka 25 iliyopita yakishuhudia kuporomoka.
Joseph Borrell kuhusiana na mgogoro huu amesema misimamo mikali ya kutofautiano inayooneshwa baina ya upande wa wazalendo na ule unaopigania kujitena inaongezeka na inahujumu uthabiti na hata mshikamano wa taifa hilo la Bosnia Herzegovina.