Mawaziri wa mambo ya nje wa EU wakutana mjini Kyiv
2 Oktoba 2023Katika taarifa yake kwenye mtandao wa kijamii, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amesema kuwa wanakutana katika mkutano huo wa kihistoria nje ya Umoja wa Ulaya nchini Ukraine aliyoitaja kuwa mwanachama wa siku zijazo wa Umoja huo, kuonesha mshikamano wao na msaada kwa watu wa nchi hiyo.
Soma pia:Mawaziri wa ulinzi wa EU wajadili msaada wa muda mrefu kwa Ukraine.
Borell ameongeza kuwa hatima ya Ukraine imo ndani ya umoja wa Ulaya. Ukraine imepongeza mkutano huo.
Mkutuno wa mawaziri wa EU nchini Ukraine ni tukio la kihistoria
Akielezea kuridhishwa kwake na mkutano huo, waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba amesema kuwa tukio hilo ni la kihistoria kwa sababu kwa mara ya kwanza kabisa, baraza la mashauri ya nchi za nje linaandaa vikao vyake nje ya mipaka ya Umoja wa Ulaya, lakini ndani ya mipaka ya siku zijazo ya Umoja huo. Kuleba ameongeza kuwa huo ni ujumbe tosha wa kuungwa mkono na wa msaada ambao Umoja wa Ulaya unatoa kwa Ukraine.
Ukraine iko katika mazungumzo na Marekani
Katika hatua nyingine, Kuleba amesema kuwa Ukraine iko katika mazungumzo na vyama vya Republican na Democratic mjini Washington kwa lengo la kupata msaada wa kuendelea wa Marekani katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi nchini humo.
Akizungumza pembezoni mwa mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Kuleba amesema hakujakuwa na ishara hadi kufikia sasa ya kusitishwa kwa msaada wa Marekani kwa Ukraine.
Soma pia: Scholz aunga mkono juhudi za amani Ukraine
Kuleba amesema Marekani inaelewa kuwa kilicho ndani ya Ukraine kiko hatarini zaidi kuliko Ukraine akimaanisha utulivu na usalama wa ulimwengu.
Mawaziri wa EU wapongeza mkutano wao nchini Ukraine
Wakati huo huo, waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi Hanke Bruins Slot amesema ni muhimu sana kukutana nchini Ukraine leo ili kuonyesha mshikamano kwa taifa hilo.
Soma pia: Ulaya yataka Marekani kufikiria upya msaada wake kwa Ukraine
Kwa upande wake, waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Catherine Colonna amesema mkutano huo wa leo ni ishara kwa Urusi kuhusu kujitolea kwa Umoja huo wa Ulaya kuiunga mkono Ukraine kwa muda mrefu. Colonna amewaambia wanahabari mjini Kiev kwamba hatua hiyo ni onyesho la maamuzi yao ya kuisaidia Ukraine hadi itakaposhinda na kwamba pia ni ujumbe kwa Urusi kutotegemea kuchoka kwa Umoja huo katika harakati zake.