1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Mawaziri wa NATO wakutana kujadili kadhia ya vita Ukraine

29 Novemba 2022

Waziri Antony Blinken na wenzake wa jumuiya ya NATO wamekusanyika nchini Romania kwa mkutano wa siku mbili kuzungumzia kuhusu msaada zaidi kwa Ukraine wakati inakabiliwa na mashambulizi ya makobora kutoka Urusi.

https://p.dw.com/p/4KDZu
Rumänien Bukarest | Treffen der NATO-Außenminister | Antony Blinken, USA
Picha: Daniel Mihailescu/AFP/Getty Images

Mkutano huo katika mji mkuu wa Bucharest huenda ukashuhudia mataifa ya jumuiya hiyo ya NATO yakitoa ahadi mpya za msaada usio na madhara kwa Ukraine kama vile  mafuta, jenereta, vifaa vya matibabu na vifaa vya msimu wa baridi.

Maafisa wa marekani wamesema kwamba nchi yao itatangaza msaada madhubuti wa gridi ya nishati ya Ukraine.

Kabla ya mkutano huo, katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema kwamba rais wa Urusi Vladmir Putin anajaribu kutumia msimu wa baridi kama silaha ya vita dhidi ya Ukraine na kwamba mataifa washirika wa NATO pamoja na Ukraine, yanapaswa kujiandaa kwa mashambulizi zaidi.

Soma pia: NATO: Uturuki iridhie uanachama wa Finland na Sweden 

Katika taarifa hii leo, Stoltenberg amesema kuwa Jumuiya hiyo haitarudi nyuma katika msaada wake kwa Ukraine na kwamba itasimama na Ukraine kwa muda utakaohitjaika huku akitoa wito kwa mataifa wanachama kutoa ahadi zaidi za msaada kwa Ukraine wakati huu wa msimu wa baridi, Ukraine inapojiandaa kwa baridi zaidi na giza kutokana na mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundo mbinu yake.

Stoltenberg ameongeza kuwa lengo kuu ni kuisaidia Ukraine na kuhakikisha rais wa Urusi Vladmiri Putin hapati ushindi katika vita hivyo. Stoltenberg pia amesema kwamba njia ya pekee ya kupata vigezo muhimu kwa mazungumzo kuanza itakuwa ni Ukraine kupata ufanisi katika uwanja huo wa vita.

Gridi ya nishati ya Ukraine imeharibiwa kote nchini humo tangu mapema mwezi Oktoba na mashambulizi ya kulengwa ya Urusi katika kile ambacho maafisa wa Marekani wamekitaja kuwa kampeini ya Urusi ya kutumia msimu wa baridi kama silaha.

Mataifa washirika binafsi pia yana uwezekano wa kutangaza usambazaji mpya wa vifaa vya kijeshi kwa Ukraine,  zaidi mifumo ya ulinzi wa anga ambayo inahitajika zaidi na Ukraine kulinda anga zake, lakini NATO kama shirika, halitashiriki katika hilo kuepuka kuhusishwa katika vita vikubwa na Urusi iliyojihami kinyuklia.

Mawaziri hao pamoja na mwenzao wa Ukraine Dmytro Kuleba, pia wataangazia masuala ya siku zijazo.

Siku ya Ijumaa, Stoltenberg alisema kuwa katika kipindi cha muda mrefu, wataisaidia Ukraine kujiondoa katika matumizi ya vifaa vya enzi ya kisovieti na kuanza kutumia vifaa vya kisasa vya kiwango na mafunzo ya jumuiya ya NATO.