1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Ulaya wanajadiliana kuhusu wakimbizi

10 Machi 2016

Mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels leo kujadili mgogoro wa wakimbizi baada ya magharibi mwa Balkan kufunga mipaka yao, na kuchochea hali mbaya ya kibinaadamu kwenye mpaka wa Macedonia.

https://p.dw.com/p/1IAJT
Griechenland Mazedonien Flüchtlinge bei Idomeni
Picha: Getty Images/AFP/L. Gouliamaki

Mkutano huo wa siku mbili utajadili masuala mbalimbali yakiwemo makubaliano kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki na kurejeshwa kwa ukanda huru wa kusafiri wa Schengen, sambamba na mpango wa mfumo wa ulinzi wa mipaka na pwani wa Umoja wa Ulaya, unaotazamwa kama hatua muhimu ya kuhakikisha ulinzi kwenye mipaka ya umoja huo.

Mazungumzo hayo yanakuja baada ya Slovenia na Croatia, mawili kati ya mataifa yaliyoko kwenye njia ya Balkan iliyotumiwa na mamia ya maelfu ya watu katika miezi ya karibuni, kuwazuwia kuitumia njia hiyo wahamiaji kuanzia usiku wa Jumatano, na Serbia kuashiria kuwa itafuata mkondo huo.

Waziri mkuu wa Slovenia Miro Cerar alisema hatua hiyo inamaanisha kuwa njia ya Balkan haipo tena kwa wahamiaji haramu, huku rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk, akisema kwwenye mtandao wake wa twitter kuwa "mmiminiko usiodhibitiwa wa wa wahamiaji kwenye njia ya Balkan umefikia mwisho."

EU Sondergipfel Türkei in Brüssel Davutoglu Tusk
Viongozi wakuu wa EU wakiwa kwenye mkutano na waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu kuhusu mgogoro wa wakimbizi mjini Brussels siku ya Jumatatu.Picha: Reuters/Y. Herman

Tusk alisema hilo siyo suala la hatua za upande mmoja lakini uamuzi wa pamoja wa mataifa 28 ya Umoja wa Ulaya, na kuyashukuru mataifa ya Balkan Magharibi kwa kutekeleza sehemu ya mkakati mpana wa Umoja wa Ulaya kushughulikia mgogoro wa wahamiaji.

Merkel apingana na kauli ya Tusk

Lakini Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ameonya Alhamisi kuwa hatua ya kufunga njia hiyo haitatuwi tatizo la wakimbizi na kwamba hatua hiyo siyo endelevu, akisisitiza katika mahojiano na kituo cha redio ya umma cha MDR, kuwa hatua zilizochukuliwa na Austria na mataifa ya Balkan ni za kwao wenyewe na siyo uamuzi wa pamoja.

Afisa wa zamani wa serikali ya Marekani ameshauri kuundwe ukanda salama kati ya Syria na Uturuki ili kutatu mgogoro huo. David V. Aguilar, aliekuwa kaimu Kamishna wa forodha na ulinzi wa mipaka, amesema mgogoro wa wakimbizi wa Kimexico nchini mwake unafanana na mgogoro wa wakimbizi wa Umoja wa Ulaya.

"Mfano mzuri utakuwa ukanda salama kati ya Utuki na Syria ambako mmiminiko wa wakimbizi na wahamiaji wa kiuchumi utashughulikiwa," alisema Aguila na kuongeza kuwa kutakuwa na juhudi kwa Umoja wa Ulaya kuanzisha mchakato wa mahojiano, kuanza kuwatambua wakimbizi halali wanaotaka kuja katika Umoja wa Ulaya, na kuchukuwa hatua dhidi ya wale wasiostahili kuingia katika Umoja wa Ulaya.

Griechenland Mazedonien Flüchtlinge bei Idomeni
Wakimbizi waliokwama mpakani mwa Ugiriki na MacedoniaPicha: Getty Images/AFP/D. Dilkoff

Maelfu waendelea kukwama

Makubaliano yaliyofikiwa na Uturuki wakati wa mkutano wa kilele na Umoja wa Ulaya siku ya Jumatatu, na ambayo yatakamilishwa Machi 17 hadi 18 yatapelekea nchi hiyo kuwachukuwa tena wahamiaji haramu wanaowasili nchini Ugiriki.

Maafisa nchini Ugiriki walisema siku ya Jumatano kuwa karibu wahamiaji 36,000 wamekwama huko, na polisi iliongeza kuwa watu wengine 4,000 hawajulikani walipo. Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa lilisema jana kuwa karibu wahamiaji 2,000 wamekwama nchini Serbia.

Wakati huo huo, zaidi ya wakimbizi 14,000 kutoka Syria na Iraq wamepiga kambi kwenye mpaka wa Ugiriki na Macedonia, wengi wao kwa wiki kadhaa. Macedonia haijamruhusu mtu yeyote kuingia katika ardhi yake tangu siku ya Jumatatu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Josephat Nyiro Charo