May aliahidi bunge kuchelewesha Brexit
26 Februari 2019May amebadilisha uamuzi wake kuhusu mkakati wa Brexit baada ya mawaziri wake wengi kutishia kujiuzulu, na wito wa kuitishwa kura ya pili ya maoni kutoka chama cha upinzani cha Labour.
Akizungumza bungeni Jumanne, May amesema akishindwa kupata uungwaji mkono wa wabunge kuhusu mkataba wake wa kujitoa Umoja wa Ulaya katika kura ya Machi 12, basi wabunge watapewa fursa ya kupiga kura nyingine Machi 13 ya kuamua kama wanataka Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya bila ya mkataba wowote. Na hilo pia wakilikataa, basi wabunge watatakiwa kupigia kura pendekezo jengine tena Machi 14 la kuuchelewesha mchakato wa Brexit kwa muda mfupi.
"Ngoja niwe muwazi, sitaki kuon Kifungu 50 kikiongezwa muda. Nguvu yetu yote tuielekeze katika kupata mkataba na kujitoa Machi 29. Kuongezwa muda zaidi ya mwisho wa Juni, itamaanisha Uingereza kushiriki uchaguzi wa Bunge la Umoja wa Ulaya. Ni ujumbe gani tutkaokuwa tunauwasilisha kwa zaidi ya watu milioni 17 waliopiga kura ya kutaka kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya miaka mitatu iliyopita?" Amesema May akiwa bungeni.
May awataka wabunge waheshimu uamuzi wa wananchi wa 2016
May amewasisitiza wabunge kumsaidia kuiunganisha tena Uingereza, kwa kutekeleza uamuzi wa wananchi walioufanya katika kura ya maoni ya Brexit mwaka 2016, wakati asilimia 52 ya raia walipopiga kura ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya.
Kiongozi wa upinzani wa chama cha Labour Jeremy Corbyn amesema ataunga mkono kura ya pili ya maoni kuhusu Brexit iwapo kama inavyotarajiwa, mpango mbadala kwa mpango wa May utakaowasilishwa na chama cha Labour bungeni utakataliwa Jumatano ijayo.
Mwezi Januari Bunge la Uingereza lilipiga kura 432-202 dhidi ya mkataba wa May wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Hali ya aina hiyo ya kushindwa kwa serikali haikuwahi kushuhudiwa katika historia nzima ya siasa za kisasa nchini humo. Na baada ya hatua hiyo, May amekuwa akiutisha Umoja wa Ulaya kwamba iwapo haitokubaliana naye juu ya mkataba wake wa kujitoa basi kuna uwezekano wa nchi yake kuondoka bila ya mkataba wowote.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre,afp,dpa
Mhariri: Sekione Kitojo