1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAngola

Mazungumzo ya amani kati ya Kongo na Rwanda yashindikana

16 Desemba 2024

Mazungumzo yaliyopangwa kufanyika Jumapili kati ya viongozi wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kumaliza mzozo wa mashariki mwa Kongo yamefutwa baada ya majadiliano kukwama.

https://p.dw.com/p/4oAQI
Rais Paul Kagame na Felix Tshisekedi
Marais wa Rwanda Paul Kagame(kulia) na Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Simon Wohlfahrt/AFP

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa ofisi ya Rais wa Angola, Joao Lourenço, mpatanishi wa Umoja wa Afrika kwa ajili ya kumaliza mzozo huo.

Serikali ya Kongo imesema kwenye taarifa yake kwamba hatua hiyo inatokana na ujumbe wa Rwanda kukataa kushiriki.

Imesema Rwanda inaitaka Kongo ifanye mazungumzo ya moja kwa moja na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Kigali na waliodhibiti eneo kubwa la mashariki mwa Kongo, tangu mwaka 2021.

Kulikuwa na matarajio makubwa kwamba mkutano huo ulioandaliwa ungemalizika kwa makubaliano ya kumaliza mgogoro.

Kagame na Tshisekedi walikutana mara ya mwisho Oktoba jijini Paris lakini hawakuzungumza moja kwa moja, huku mazungumzo yao yakiendelea kupitia upatanishi wa Luanda.