1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan Kusini

Mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini yaanza tena

5 Desemba 2024

Mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini yaliyopewa jina la Tumaini yalianza tena jana Jumatano nchini Kenya baada ya kukwama kwa miezi minne iliyopita na pia kufutwa kazi kwa ujumbe wa serikali katika mazungumzo hayo.

https://p.dw.com/p/4nlkh
Sudan | Donald Booth | Mazungumzo ya amani
Mkuu wa ujumbe wa waasi wa Sudan, Taban Deng (katikati) akiwa na mjumbe wa Marekani kwa Sudan na Sudan Kusini Donald E. Booth (kulia) wakati wa mazungumzo mjini Addis Ababa kujaribu kumaliza vita.Picha: Solan Gemechu/AFP/Getty Images

Hizi ni juhudi za hivi karibuni zaidi za kuumaliza mzozo huo ambao kwa muda mrefu umedumaza uchumi wa nchi hiyo.

Hapo jana, mpatanishi mkuu katika mazungumzo hayo Lazarus Sumbeiyo alizitaka pande husika kati ya serikali na makundi ya upinzani ambayo hayakuwa sehemu ya makubaliano ya mwaka 2018 yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, kushughulikia masuala yaliobakia.

Soma pia: Uhalifu mpya wa kivita waripotiwa Sudan Kusini 

Mkuu wa Muungano wa Upinzani wa Sudan Kusini, Pagan Amum, aliutaka ujumbe mpya wa serikali katika mazungumzo hayo kuzingatia kile ambacho tayari kimekubaliwa na kusema ni muhimu kukumbuka kwamba pengine hiyo ndiyo fursa ya mwisho ya kuikoa nchi hiyo kutosambaratika kabisa.

Kwa upande wake, Kuol Manyang Juuk, kutoka upande wa serikali, azihimiza pande hizo husika kuweka kando tofauti zao.