1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kusitisha vita vya Israel na Hamas yanaendela

Angela Mdungu
16 Novemba 2023

Mazungumzo ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza na kuachiliwa kwa wanawake na watoto wanaoshikiliwa mateka na kundi la Hamas yanaendelea kulingana vyanzo vyenye taarifa na suala hilo.

https://p.dw.com/p/4YtDv
Vikosi vya Israel (IDF) vikiendelea kusonga mbele ndani ya Ukanda wa Gaza
Wanajeshi wa Israel katika operesheni ya ardhini Ukanda wa GazaPicha: Israel Defense Forces/Handout via REUTERS

Makubaliano hayo ya kuwaachilia baadhi ya mateka yanatarajiwa kufanikisha kusimamishwa kwa mapigano kwa siku 3 hadi tano, kuongezwa kwa misaada ya kiutu pamoja na kuachiliwa kwa wanawake na watoto wanaoshikiliwa kwenye magereza ya Israel.

Kwa mujibu wa vyanzo vyenye ufahamu na mazungumzo hayo, kundi la Hamas limekubaliana na masuala yaliyoainishwa likiwemo la kuwaachia wanawake 50 wanaoshikiliwa mateka na watoto. Kwa kufanya hivyo, Hamas itawaachilia wanawake na watoto  75 wa Kipalestina.

Soma zaidi: Israel yashambulia makaazi ya kiongozi wa Hamas

Mkuu wa kamisheni ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk ameonya kwamba ukosefu wa nishati unazuia usambazaji wa misaada na pande zote za mzozo huo haziwezi kuyaita mauaji ya raia kuwa ni ya bahati mbaya.

Mamia ya raia wa nchi za kigeni kuondoka Gaza

Karibu raia 800 wa kigeni na Wapalestina wenye pasi za kusafiria za nchi nyingine wanatarajiwa kuondoka leo Alhamisi kwenye Ukanda wa Gaza. Kulingana na shirika la hilali nyekundu la Misri zaidi ya raia 200 kati ya hao tayari walishawasili upande wa Misri wa mpaka wa Rafah.

Ukandawa Gaza| Wapalestina wakitafuta hifadhi dhidi ya mashambulizi kwenye jengo la UNRWA
Wakazi wa Gaza waliojihifadhi kwenye jengo la UNRWAPicha: Ashraf Amra/AA/picture alliance

Kwa mujibu wa orodha ya mamlaka ya mpaka ya Palestina, watu hao wana pasi za kusafiria za Urusi, Belarus, Bosnia-Herzegovina, Austria, Switzerland, Uhispania, Sweden, Norway na Marekani na nchi nyingine.

Jeshi la Israel limesema kuwa linaidhibit bandari ya mji wa Gaza kaskazini mwa ukanda huo. Jeshi hilo limesema   wapiganaji 10 wa Hamas waliuwawa kwenye Bandari hiyo awali ilikuwa ikidhibitiwa na kundi la Hamas linaloitawala Gaza. Israel imeongeza kuwa mahandaki 10 na miundombinu mingine ya kundi hilo imeangamizwa wakati wa operesheni hiyo.

Tukisalia kwenye mzozo huo, washambuliaji watatu wa Kipalestina wameripotiwa kuuwawa leo katika kituo cha ukaguzi cha kijeshi kusini mwa mji wa Jerusalem. Katika tukio hilo, watu wengine wanne wamejeruhiwa na mmoja kati ya hao yuko kwenye hali mbaya.