mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Iran yakaribia ufumbuzi
10 Julai 2015Mazungumzo yaliyoanza tena mjini Vienna ya mpango wa nyuklia wa Iran yanatimiza siku ya kumi na nne leo., ikiwa bado hatima yake haitambuliki. Mazungumzo hayo yanaitaka Iran kukubali kupunguza shughuli zake za nyuklia, ili iondoshewe vikwazo ilivyowekewa vya kiuchumi.
Muda wa mwisho wa kuwasilisha makubaliano katika bunge la Marekani - Congress ilikuwa leo asubuhi. Hata hivyo walioshiriki katika mazungumzo hayo walishindwa kulifanikisha hilo. Jambo ambalo litarefusha muda wa bunge hilo, kupitia makubaliano yatakayofikiwa kuwa siku sitini . Hili pia litachelewesha Iran kuondolewa vikwazo ilivyowekewa, hapo makubaliano yatakapofikiwa.
Hata hivyo waziri wa mambo ya nchi za nje Philip Hammond amesema mazungumzo yanapiga hatua.
“Tunasonga mbele, ingawa polepole mno kama ilivyoenekana katika hii wiki nzima iliyopita lakini tunapiga hatua. Kuna masuala ambayo yanahitaji kupatiwa ufumbuzi. Nina hakika maafisa wetu wanaofanya kazi pamoja na Iran katika masaa 12 yajayo watapata ufumbuzi na baadae mawaziri wote watakutana kesho kujadili vizuwizi vilivyobaki,” amesema Philip Hammond.
Iran yailaumu Marekani kwa mapendekezo ya kupindukia
Kwa upande wa Iran waziri wa nchi za nje Javad Zarif ameilaumu Marekani kuwa inabadilisha mapendekezo yake ya awali, na mapendekezo mengine ni ya kupindukia.
Zarif pia amepuuzia tishio la wazri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, kuwa anaweza kundoka katika meza ya mazungumzo hayo kama ni tishio lisilo na tija.
Kerry alisema kuwa mazungumzo hayo hayatoharakishwa, lakini pia hayataweza kuendelea milele. Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Moghrini, amesema pia wakati umefika wa kupatikana makubaliano mazungumzo hayo ya mpango wa nyuklia wa Iran.
Mogherini amekiambia kituo cha televisheni cha CNN kuwa makubaliano yapo yanakaribia, lakini kama hakujafanywa maamuzi muhimu na ya kihistoria katika masaa machache yajayo basi makubaliano ya kudumu hayatafikiwa.
Mazungumzo hayo juu ya mpango wa nyuklia wa Iran yanajumuuisha pande mbili. Upande wa mataifa sita yenye nguvu duaniani Uingereza, Uchina, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Marekani pamoja na upande wa Iran. Pande ambazo zimekuwa zikijadiliana kwa mika kumi na tatu sasa, kuikubalisha Iran iachane na mpango wake wa silaha za nyuklia ili iondolewe vikwazo bvya kiuchumi.
Moja ya kikwazo kikubwa cha kufikiwa makubaliano, ni Iran kukataa ukaguzi wa Umoja wa Matifa katika kambi zake za kijeshi. Iran imesema, inahofia hii itakuwa ni njia kwa Marekani kuifanyia upelelezi.
Mwandishi: Yusra Buwayhid / afpe/ape/
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman