Mazungumzo ya muafaka wa Brexit Uingereza yavunjika
18 Mei 2019Kiongozi wa chama cha labour Jeremy Corbyn amesema mpasuko kati yao hauwezi kuzibwa, na ile hali ya kujiamini haipo tena kwamba mrithi wake ataendelea na maridhiano yoyote yanayoweza kupatikana. Majadilino "yamekwenda hadi yalipofikia," Corbyn amesema katika barua kwa May.
"Ongezeko la udhaifu na kutokuwa thabiti kwa serikali yako kuna maana hakutakuwa na imani katika kulinda chochote kinachoweza kukubaliwa baina yetu," amesema.
Corbyn amesema chama cha Labour kwa hiyo kitaendelea kupinga makubaliano ya taalka yaliyofikiwa na serikali kama yalivyo hivi sasa.
Wabunge mara tatu waliyakataa makubaliano yaliyofikiwa na May pamoja na Umoja wa Ulaya, na kumlazimisha kuchelewesha tarehe ya Brexit mara mbili na kukinyooshea mkono chama cha Labour.
Muda mpya wa mwisho ni Oktoba 31.
Bunge linatarajiwa kupiga kura kwa mara ya nne mapema mwezi Juni kuhusiana na masharti ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya.
May anaonekana kuchoka
May ambaye ameonekana kuchoka alisema wabunge watakabiliwa na kile alichosema kuwa ni " chaguo gumu": kupiga kura kukubaliana na Brexit , ama "kukataa tena".
Alikuwa akizungumza katika tukio mahsusi la kampeni kabla ya uchaguzi wa bunge la Ulaya, utakaofanyika nchini Uingereza siku ya Alhamis, ambapo maoni ya wapiga kura yanaonesha chama chake cha Conservative kinaweza kushika nafasi ya tano.
Uingereza haikutaka kushiriki katika uchaguzi huo lakini itafanya hivyo kwasababu ya kuahirishwa kwa Brexit.
Kuvunjika kwa mazungumzo hayo kumekuja siku moja baada ya May kukubali kuweka muda maalum kwa ajili ya kuachia wadhifa wa uwaziri mkuu kufuatia kura ya kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya bungeni, ambayo itafanyika katika muda wa wiki moja kuanzia Juni 3. Makubaliano hayo yamefikiwa katika mkutano wa faragha pamoja na wanachama na viongozi wa wabunge wa chama cha Conservative.
Inafikiriwa kwamba May atazindua mpambano wa kuwania nafasi ya uongozi mara mswada wa makubaliano ya kujitoa ama ukishindwa, kama inavyoonekana kuwa , ama utakamilishwa.
Mwandishi: Sekione Kitojo