Mazungumzo ya nyuklia yaongezwa muda
30 Juni 2015Iran na nchi sita zenye nguvu duaniani ambazo ni Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, China, Urusi pamoja na Marekani wamerudi tena katika meza ya mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Iran leo hii. Pande hizo mbili zimekubaliana mazungumzo kuengezewa muda, ikiwa siku ya mwisho ya kufikiwa makubalaino ilikuwa iwe leo.
Pande zote mbili zinasema zinafahamu kuwa kuna vikwazo vikubwa vya kukabiliana navyo, kabla ya kupata makubaliano ya kudumu.
Makubaliano hayo yatailazimu Iran kupunguza shughuli zake za kinyuklia, ili iweze kuondolewa vikwazo ilivyowekewa kwa zaidi ya muongo moja sasa.
Wanadiplomasia wamesema muda wa mwisho wa kufikia makubaliano kwa hakika sio Juni 30, bali ni Julai 9. Hii ikiwa ndio siku ya mwisho, kwa makubaliano hayo kuwasilishwa katika bunge la Marekani - Congress. Na baada ya kipindi cha siku 30 cha mapitio ya makubaliano hayo, rais Obama wa Marekani ataondoa vikwazo dhidi ya Iran.
Hata hivyo wanadiplomasia hao wamependekeza muda wa mapitio urefushwe hadi siku 60, kuondoa wasiwasi kuwa makubaliano hayo huenda yakavunjwa.
Tafauti kubwa baina ya pande hizo mbili, ni juu ya kasi na muda utakaochukua hadi vikwazo dhidi ya Iran kuondolewa. Pamoja na madai ya nchi za magharibi kuwa lazima Umoja wa Mataifa ufanye ukaguzi wa kambi za kijeshi, pamoja na maabara za wanasanyansi wa teknolojia ya nyuklia. Jambo ambalo Iran hadi sasa hakubaliani nalo.
Nchi za magharibi na Netanyahu waishutumu Iran
Nchi za magharibi na washirika wake wanaishutumu Iran kuwa huenda ikawa inakuza teknologia ya nishati ya nyuklia, ambayo itaiwezesha kuunda silaha za nyuklia. Na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu leo amesisitiza kuwa mpango unaojadiliwa baina ya Iran na nchi hizo sita, utaipa nafasi nchi hiyo kutengeza silaha za kinyuklia. Hata hivyo Iran inakana shutuma hizo, na kusema shughuli zao za teknologia ya nyuklia ni za salama.
Netanyahu anasema kuinuliwa vikwazo kwa Iran, kutairuhusu kukusanya mabilioni ya fedha na kuiwezesha nchi hio kuendelea na mpango wake wa kigaidi wa kuunda mabomu ya nyuklia.
Maafisa wa Marekani wamesema nchi hizo sita zenye nguvu duniani zitahakikisha kuwa Shrirka la Nishati ya Kinyuklia la Kimataifa (IAEA), linafanya ukaguzi katika maabara za nishati ya nyuklia pamoja na kambi za kijeshi za Iran. Hata hivyo hivi karibuni Kiongozi mkuu wa Iran ayatollah, Ali Khamenei, alisema nchi yake haitokubali maeneo yake ya kijeshi kukaguliwa.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman