1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbinu zisizorasmi zilizotumiwa na CIA kuwahoji washukiwa wa ugaidi zachapishwa hadharani

17 Aprili 2009

Utawala wa Rais Barack Obama umezifungua nyaraka zote na kuweka hadharani mbinu zilizotumiwa na utawala wa Rais George Bush, kuwahoji washukiwa wa ugaidi.

https://p.dw.com/p/HYu5
Washukiwa wa ugaidi, huko Guantanamo Bay.Picha: AP / DW

Obama hata hivyo amewahakikishia maafisa wa shirika la kijaasusi la CIA waliohusika kuwa hawatochukuliwa hatua za kisheria.


Katika nyaraka zilizochapishwa jana maafisa wa kisheria katika utawala wa Bush walijitetea kwamba mbinu walizozitumia kama kumpiga mshukiwa makofi, kutumia wadudu kuwatisha washukiwa na kuwakosesha usingizi ili wakiri wanayotuhumiwa, haikuwa mateso.


Rais Obama hata hivyo alikuwa mwepesi kuwahakikishia maafisa wa CIA waliohusika kuwahoji washukiwa hao wa ugaidi, kwamba hawatochukuliwa hatua za kisheria. Huu ni wakati wa kujirudi na kurekebisha makosa, wala si wakati wa kuadhibu, Alisema Obama.


Aliongeza kwamba,maafisa hao walikuwa tu wanafuata maagizo na wametumikia taifa lao kwa moyo wao wote.


USA Guantanamo Gefangerner in Handschellen
Mshukiwa wa ugaidi akiwa amefungwa minyororo huko Guantanamo BayPicha: AP

Nyaraka hizo nne zilizotolewa wazi, zilifichua mbinu walizozitumia maafisa wa CIA katika walipowakamata na kuwahoji washukiwa wa ugaidi katika mpango uliaoanzishwa punde tu baada ya yale mashambulizi ya Septemba 11 nchini Marekani.


Wakosoaji wameshikilia kwamba mbinu hizi zilizotumika zilikuwa ni mateso, huku Obama akizitaja mbinu hizi kama ukiukaji wa maadili ya kibinadamu na aibu kwa Marekani.


Anthony Romero, mkurugenzi mtendaji wa kitengo kinachosimamia mfumo wa sheria Marekani, amesema kwamba Marekani ili kupiga hatua mbele kwanza iyatizame yaliyopita katika utawala wa Bush na kurekebisha.


Maafisa wa Bush, nao walisisitiza mbinu zote walizozitumia hazikuwaathiri kiakili wala kiafya washukiwa, hivyo haziwezi kuorodheshwa kama mbinu za mateso.


Nyaraka hizi zilifichua kinaganaga matumizi kama vile, kulazimishwa kukaa uchi, kuzabwa makofi ya uso na tumbo na washukiwa wa kulazimishwa kufungiwa katika maeneo madogo yasio na nafasi kama njia za kuwafanya wakiri makosa.


BdT Nachstellung eines Guantanamo Gefangenen am Tag gegen die Folter der UNO London Großbritannien
Mshukiwa wa ugaidi, kafunikwa uso na karatasi ya nailoni.Picha: AP

Washukiwa wengine wa Al-Qaeda huko Guantanamo Bay walifungiwa ndani ya vyumba vidogo, na ndani kuwekwa wadudu wa kutisha. Mbinu zingine zilizotumiwa na ambazo zimeelezwa katika nyaraka hizi ni kwa maafisa wa CIA kuwafunika nyuso washukiwa na kisha kutumbukiza vichwa vyao nda ni ya maji, mithili wanataka kuwazamisha.


Wengine walifunikwa nyuso na miguu yao kufungwa na minyororo.


Utawala wa Obama hata hivyo umeshtumiwa na makundi ya kutetea haki za kibinadamu, kwa hatua yake ya kutowachukuliwa hatua za kisheria maafisa wa CIA waliohusika katika visa hivi. Shirika la Amnesty limehoji hatua ya utawala wa Obama, likisema maafisa wa utawala wa Obama wamekubali njia hizi zilizotumika zilikuwa mateso, kwa hivyo kwanini maafisa waliohusika hawafunguliwi mashtaka.


Mwandishi Munira Mohammed/ AFP

Mhariri Saumu Mwasimba