1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mechi za Kenya kufuzu kombe la dunia zahamishiwa Malawi

16 Mei 2024

Mechi mbili za Kenya za kufuzu kwa Kombe la Dunia la mwaka 2026 zimehamishiwa Malawi baada ya serikali kufunga viwanja vyote vikuu, hatua ambayo pia inaathiri maandalizi ya riadha kabla ya Michezo ya Olimpiki ya Paris.

https://p.dw.com/p/4fuuK
Kenya Nairobi
Uwanja wa Nyayo jijini NairobiPicha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

Mechi mbili za Kenya za kufuzu kwa Kombe la Dunia la mwaka 2026 zimehamishiwa Malawi baada ya serikali kufunga viwanja vyote vikuu, hatua ambayo pia inaathiri maandalizi ya riadha kabla ya Michezo ya Olimpiki ya Paris.

Ratiba muhimu ya kandanda ya Kundi F dhidi ya Burundi na mabingwa wa Afrika Ivory Coast sasa itafanyika katika uwanja wa taifa wa Bingu mjini Lilongwe mwezi ujao. Kenya kuwasilisha ombi la pamoja la kuwa mwenyeji wa AFCON2027

Wizara ya michezo ya Kenya ilitangaza kuwa mwezi Aprili itafunga viwanja viwili vikuu vya Nairobi na kingine katika kitovu cha riadha cha Eldoret kwa ukarabati ili kujiandaa kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2027 ambalo Kenya itakuwa mwenyeji kwa pamoja na Tanzania na Uganda.

Msemaji wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) amesema amewasiliana na mwenzake wa Malawi ambaye alikubali kuandaa michuano hiyo miwili ya Kombe la Dunia kutokana na ukosefu wa viwanja vilivyoidhinishwa na FIFA jijini Nairobi.

Waziri wa Michezo wa Kenya Ababu Namwamba alitetea hatua hiyo akisema kuna umuhimu wa kurekebisha vifaa vya michezo nchini humo "ambavyo vimetelekezwa na kushughulikiwa kwa kawaida sana".