1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani kuunda serikali Ugiriki

Mohammed Khelef21 Agosti 2015

Siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras, kutangaza kujiuzulu, kiongozi wa upinzani, Evangelos Meimarakis, amesema hivi leo kuwa atafanya kila awezalo kuunda serikali mpya ili kuepuka uchaguzi wa mapema

https://p.dw.com/p/1GJJo
Kiongozi wa chama cha kihafidhina cha New Democracy, Evangelos Meimarakis, amepewa jukumu la kuunda serikali mpya Ugiriki.Evangelos Meimarakis
Kiongozi wa chama cha kihafidhina cha New Democracy, Evangelos Meimarakis, amepewa jukumu la kuunda serikali mpya Ugiriki.Picha: dapd

Meimarakis, anayeongoza chama cha New Democracy, alikabidhiwa rasmi jukumu la kuunda serikali mpya mapema leo na Rais Prokopis Pavlopoulus, na mara tu baada ya kutoka kwenye kasri ya rais huyo, amewaambia waandishi wa habari kuwa uchaguzi wa mapema uliokuwa umepangwa kufayika tarehe 20 Septemba, hauna maana, na badala yake atajaribu kuunda serikali kuepuka athari mbaya na za muda mrefu ambazo zinaweza kusababishwa na uchaguzi huo.

"Kama mujuavyo, tayari nimekutana na Rais wa Jamhuri ambaye amenipa idhini ya siku tatu kuchunguza ikiwa bunge linaweza kutupa imani ya kuunda serikali mpya. Hivyo, nitakutana na spika wa bunge kumshawishi kuitisha mkutano wa viongozi wa vyama ili kupata suluhisho la kuepuka madhara ya uchaguzi wa mapema, ambao naamini hauna faida yoyote," alisema Meimarakis.

Kiongozi huyo mhafidhina ana siku tatu tu za kusaka washirika wa kuunda serikali ya mseto. Endapo atashindwa ndani ya masaa haya 72, atalazimika kuirejesha ridhaa hiyo kwa rais mwenyewe, ambaye naye atakipatia nafasi hiyo chama cha tatu kwa ukubwa, ambacho kinaundwa na kundi lenye msimamo mkali zaidi lililohama muungano wa mrengo wa shoto wa waziri mkuu aliyejiuzulu, Tsipras. Kundi hilo linalojiita Popular Unity linaundwa na wabunge 25 wakiongozwa na waziri wa zamani wa nishati, Panagiotis Lafazanis.

Upinzani dhaifu, Tsipras dhaifu

Hata hivyo, wachunguzi wa mambo wanasema upinzani una fursa ndogo sana ya kuungana na kuunda serikali ya pamoja kwa haraka kiasi hicho, jambo linalomaanisha kuwa hata baada ya miaka mitano ya kuzidi kudhoofika kiuchumi, taifa hilo linaelekea kwenye uchaguzi wake wa tano.

Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Alexis Tsipras.
Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Alexis Tsipras.Picha: Reuters/F. Lenoir

Kujiuzulu ghafla kwa Tsipras hapo jana na kuitisha uchaguzi wa mapema mwezi ujao kulikusudiwa kumpa wasaa wa kuwashughulikia waasi kwenye chama chake, ambao hawakubaliani na awamu ya tatu ya mkopo wa fedha kwa nchi hiyo kutoka kwa wakopeshaji wa kimataifa.

Kwa upande mwengine, hata kama wapinzani wakishindwa kuungana na hivyo Tsipras kufanikiwa kuitisha uchaguzi wa mwezi ujao, uwezekano wa yeye kuibuka na ushindi wa moja kwa moja ni mdogo na, hivyo, atapaswa tena kusaka uungwaji mkono wa wapinzani wake kuunda serikali ambayo itamnyima nguvu za kutekeleza mageuzi ya kiuchumi na kisera anayoyapigania sasa.

Katika kila hali, Ugiriki imekwama.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga