Meli ya Ukraine iliyobeba ngano yaelekea Misri
22 Septemba 2023Meli ya pili iliyobeba shehena ya ngano, imeng'oa nanga kutoka bandari ya Chornomorsk ya Ukraine kwenye Bahari Nyeusi ikiwa imebeba takriban tani 20,000 za nafaka. Hayo yamesemwa leo Ijumaa na waziri wa miundo mbinu wa Ukraine Oleksandr Kubrakov.
Hiyo ni meli ya pili yenye nafaka kutoka Ukraine tangu Urusi iliporudisha vizuizi dhidi ya safari kupitia Bahari Nyeusi mwezi Julai.
Meli hiyo imebeba ngano zinazopelekwa katika nchi za Asia na Afrika.
Baada ya Urusi kujiondoa kwenye mkataba wa mauzo ya nafaka unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Ukraine inajaribu njia mpya ya baharini inayoepuka njia kuu. Badala yake inafuata njia zinazodhibitiwa na wanachama wa NATO, Bulgaria na Romania.
Hapo awali Kyiv ilifanikiwa kutuma meli kadhaa za shehena kwenye njia hiyo mpya, bila kusafirisha nafaka zake.
Meli ya kwanza iliyobeba tani 3,000 za ngano iliondoka katika bandari hiyo mapema wiki hii.