1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ahimiza umoja katika kupambana na korona

Daniel Gakuba
18 Juni 2020

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema janga la virusi vya korona limeanika kweupe udhaifu katika Umoja wa Ulaya, wakati ambapo nchi za umoja huo zilihitaji mshikamano kuliko wakati mwingine.

https://p.dw.com/p/3e0A9
Deutschland | Bundeskanzlerin Angela Merkel hält eine Rede vor dem Bundestag in Berlin
Angela Merkel, Kansela wa UjerumaniPicha: Reuters/A. Hilse

 

Katika hotuba yake mbele ya bunge mjini Berlin Alhamis, Kansela Merkel ameangazia masuala yanayotazamiwa kuwa yenye kimpaumbele mnamo kipindi cha miezi sita ambapo Ujerumani itakuwa rais wa baraza la umoja huo. Amesema virusi vya korona vimekuwa changamoto kubwa zaidi kwa Umoja wa Ulaya tangu kuundwa kwake, na vimedhihirisha kuwa msingi wa umoja hau bado haujaimarika.

Bi Merkel amesema badala ya kushirikiana kutafuta suluhu ya pamoja baada ya janga la COVID-19 kubisha hodi, kila nchi ilijitazama yenyewe.

Kila nchi ilijitazama kivyake

''Tunapaswa kukiri kwamba janga hili limemulika udhaifu wa mradi wa Umoja wa Ulaya. Lililpozuka, fikra ya kwanza ya kila nchi, ikiwemo yetu ya Ujerumani, ilikuwa kujijali kama taifa''. Amesema Merkel. 

''Hili, hata kama lilitokana na nia njema'', amesisitiza kansela huyo, '' halikuwa sahihi, kwa sababu janga la kidunia, linahitaji kushughulikiwa kwa juhudi za kimataifa, kwa kuungana mkono.''

Bi Merkel amesema janga la korona limeonyesha kuwa Ulaya inapaswa kujitwisha majukumu ya kidunia, kwa sababu viongozi wa kiimla wanataka kulitumia kujinufaisha.

Deutscher Bundestag Plenum Sitzung in Berlin
Bundestag, Bunge la Shirikisho la Ujerumani mjini BerlinPicha: picture-alliance/Flashpic/J. Krick

''Wanataka kuuhujumu utawala wa sheria, na kukandamiza heshima ya ubinadamu, haki za binadamu na haki za kiraia'', amesema Bi Merkel katika hotuba yake.

Kiongozi huyo amezungumzia pia kuenea kwa habari za kupotosha, ambako amesema ni changamoto ya kidunia inayoukabili Umoja wa Ulaya, na kutaka nchi za umoja huo kusimama kidete kupambana na kadhia hiyo, hata nje ya mipaka yao.

Mwiba katika uhusiano na China

Amezungumzia vile vile uhusiano baina ya Ulaya na China ambao amesema litakuwa suala muhimu wakati wa urais wa Ujerumani katika baraza la Ulaya, akisema Ujerumani inaunga mkono mjadala wenye uwazi. Amezitaka nchi za Ulaya kuzungumza kwa sauti moja katika mjadala huo, hususan kuhusiana na suala la Hong Kong.

Mada nyingine zilizoangaziwa katika hotuba ya Bi Merkel ni mfumo wa kidijitali, na kuhamia katika uchumi ambao ni rafiki kwa mazingira.

Hotuba hiyo ameitoa siku moja kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya, ambao utalenga kukubaliana juu ya bajeti ya umoja huo kwa miaka kadhaa ijayo.

Hata hivyo, alipozungumza na kundi la wabunge kutoka vyama vya kihafidhina mapema wiki hii, Kansela Angela Merkel alisema hatarajia kuwa muafaka kuhusu bajeti hiyo utafikiwa kabla ya mwisho wa mwezi Julai.

Ujerumani itakuwa rais wa baraza la Umoja wa Ulaya kuanzia Julai mosi, hadi mwishoni mwa mwaka huu wa 2020.

 

dpae, afpe