Merkel aitaka Ulaya kupinga wanasiasa wanaonunulika
19 Mei 2019Hii ni baada ya tukio la kamera iliyofichwa kumwangusha makamu kansela wa Austria Heinz-Christian Strache kuhusiana na madai kwamba ana kubali rushwa.
Wakati vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vimekataa maadili kama kuwalinda watu waliowachache pamoja na haki za msingi za binadamu , Merkel aliwaambia waandishi habari katika mji mkuu wa Croatia , Zagreb , kwamba "wanasiasa ambao wanaweza kununuliwa wanawajibika, na tunapaswa kuchukua hatua kamili dhidi ya yote hayo".
Magazeti ya Ujerumani ya Der Spiegel na Sueddeutsche Zeitung jioni ya Ijumaa yalichapisha vidio iliyorekodiwa, ikidaiwa kumuonesha kiongozi wa chama cha Fredom Party (FPOe) Strache akiahidi mikataba wa serikali ili kuweza kupata msaada katika kampeni kutoka kwa mfanyakazi wa benki bandia kutoka Urusi.
Merkel , mwanasiasa mwenye uzito katika kundi la vyama vya siasa za wastani za mrengo wa kulia katika mataifa ya Umoja wa Ulaya EPP, alikuwa akizungumza kabla ya mkutano wa chama cha kihafidhina nchini Croatia cha HDZ wakati kampeni za uchaguzi wa bunge la Ulaya zikifikia mwisho.
Adui wa mradi wa Ulaya
Akizungumza kwa ukakamavu kabisa katika tukio hilo la kampeni, amedai kwamba "uzalendo na mradi wa Ulaya havikinzani".
"Lakini siasa za kizalendo ni adui wa mradi wa Ulaya, na tunapaswa kuweka wazi hilo katika siku za mwisho kabla ya uchaguzi," ameongeza.
Kuingilia kati kwa Merkel kunafuatia wimbi la miito kutoka wanasiasa viongozi wa Ujerumani kwa wapiga kura kutofuata mfano wa nchi jirani kwa kuwaweka wanasiasa wenye misimamo wa siasa kali za mrengo wa kulia katika nafasi za madaraka.
Kansela mhafidhina wa Austria Sebastian Kurz amekuwa ni mtu ambaye hajaonesha uwajibikaji kwa kukikaribisha chama cha FPOe katika serikali yake , waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto Social Democratic SPD amesema, akiwaita "maadui wa uhuru".
Wengine moja kwa moja wamekionya chama cha CDU kuachana na uwezekano wa ushirikiano na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ujerumani cha Alternative for Germany , AfD.
Wapiga kura baadaye mwaka huu katika eneo la zamani mashariki mwa Ujerumani lililokuwa la kikomunist wanatarajiwa kukipa chama hicho matokeo mazuri hali inayoweza kuwa vigumu kujenga serikali ya mseto katika ngazi ya taifa bila chama hicho.
Vyama vya siasa za wastani vya mrengo wa kulia katika bara la Ulaya "vinapaswa kuacha ushirika wao na vyama vya mrengo wa kulia na kujiweka mbali kwa uwazi na maadui wa demokrasia," mgombea wa chama cha kijani kwa ajili ya bunge la Ulaya Sven Giegold ameyaambia magazeti ya kundi la Funke.