Merkel akutana na Tsipras
24 Machi 2015Kansela Merkel na Tsipras walikuwa na mazungumzo ya kina yaliyodumu kwa muda wa saa tano mjini Berlein, ambayo yameonekana kuwa ya kujenga katika mazingira ya kirafiki, huku wakisisitiza nia yao ya kuondoa mvutano uliopo kati ya serikali zao. Viongozi hao wamezungumzia kuhusu hali ya kiuchumi ya Ugiriki, utaratibu wa Umoja wa Ulaya na mustakabali wa ushirikiano kati ya Ugiriki na Ujerumani.
Akizungumza katika mkutano wake na Tsipras na waandishi wa habari, Merkel amesema licha ya tofauti zilizopo sasa kuhusu mpango wa uokozi kuisaidia Ugiriki isifilisike kiuchumi pamoja na masuala mengine kadhaa, nchi zao zimeendelea kubakia washirika wa karibu, huku wakiwa na uhusiano mzuri kisiasa na kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili ni muhimu.
''Nataka kusisitiza wazi kuwa Ujerumani ina uhusiano wa karibu na kirafiki na Ugiriki pamoja na watu wa Ugiriki. Kuna watu wengi wanaoishi Ujerumani ambao wana asili ya Kigiriki,'' alisema Merkel.
Kwa upande wake Tsipras ambaye anazuru rasmi Ujerumani kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani mwezi Januari mwaka huu, ameonyesha kuwa nchi yake bado inatafuta masharti nafuu yatakayosaidia kuunusuru uchumi wake.
Tsipras kuzingatia mafanikio yaliyopatikana
''Hatutaki kuharibu mafanikio yaliyopatikana miaka mitano iliyopita. Tunahitaji kutekeleza mageuzi ambayo awali serikali zilizotangulia, zilishindwa kuyafikia, mageuzi ya kodi, hatua za kupambana na rushwa pamoja na ukwepaji wa kulipa kodi,'' alifafanua Tsipras.
Uhusiano kati ya Ujerumani na Ugiriki uliingia dosari tangu Tsipras na serikali yake inayoongozwa na chama cha Syriza kuingia madarakani na kuendeleza sera yake ya kupinga vikali masharti magumu ya kubana matumizi.
Kansela Merkel amesema uamuzi wowote kuhusu suluhisho la matatizo ya kifedha yanayoikumba Ugiriki utapatikana tu kutoka kwa mataifa yote yanayotumia sarafu ya Euro. Wiki ijayo serikali mpya ya Ugiriki inatarajia kuwasilisha orodha yake ya mageuzi ya kiuchumi.
Asubuhi hii, Tsipras atakutana na viongozi wa chama cha upinzani cha siasa kali za mrengo wa kushoto-Die Linke, Katja Kipping na Gregor Gysi, ambapo majira ya mchana anatarajiwa kukutana na viongozi wa chama cha Kijani, Cem Özdemir na Simone Peter.
Baadae, waziri huyo mkuu wa Ugiriki, atatembelea makumbusho ya mauwaji yaliyofanywa na utawala wa Wanazi dhidi ya Wayahudi, Holocaust mjini Berlin, hatua ambayo inaelezwa huenda ikatilia mkazo madai ya serikali yake ya kutaka kulipwa fidia, ambayo Tsipras ameyaita kama ''suala la kimaadili.''
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,RTRE
Mhariri: Iddi Ssessanga