Merkel apigania usalama zaidi wa mawasiliano
17 Februari 2014Merkel amesema Jumamosi (15.02.2014)atazungumza na Rais Francois Hollande wa Ufaransa juu ya kutengeneza mtandao huo wa mawasiliano wa Ulaya kufuatia kuzuka kwa wasi wasi mkubwa barani Ulaya baada ya kuvuja kwa nyaraka za siri za Shirika la Upelelezi la Marekani NSA mwaka jana kulikobainisha kupelelezwa na shirika hilo kwa mawasiliano ya umma mkubwa wa wananchi wa Ulaya bila ya ridhaa yao.
Merkel ambaye anaizuru Ufaransa hapo Jumatano amekuwa akishinikiza kuwepo kwa ulinzi mkubwa wa data barani Ulaya kufuatia repoti hizo za kupelelezwa kwa mawasiliano hayo nchini Ujerumani na kwengineko.Hata simu ya mkono ya Merkel ilikuwa ikipelelezwa na makachero wa Marekani.
Merkel amesema katika hotuba yake ya kila wiki kwa njia ya mtandao kwamba hapendelei kwa makampuni ya mtandao kama vile Google na Facebook kuwa na makao makuu ya operesheni zao katika nchi zenye viwango vya chini vya ulinzi wa data wakati harakati zao kubwa zikiwa katika nchi kama Ujerumani ambayo ina kiwango cha juu cha ulinzi wa data.
Ulinzi wa data wa hali ya juu
Merkel amekaririwa akisema " Tutazungumza na Ufaransa juu ya vipi tutaweza kudumisha ulinzi wa data wa hali ya juu."
Ameongeza kusema "Ziada ya yote hayo tutazungumza na makampuni ya Ulaya ambayo yanashughulikia usalama wa wananchi wetu ili kwamba mtu asilazimike kutuma baruwa pepe na taarifa nyengine kupitia Marekani na badala yake kutengenezwe mfumo wa mawasiliano ya mtandao ndani ya bara la Ulaya."
Ofisi ya Rais Hollande wa Ufaransa imethibitisha kwamba serikali za nchi hizo mbili zimekuwa zikilijadili suala hilo na kwamba serikali ya Ufaransa inakubaliana na mapendekezo ya serikali ya Ujerumani.
Afisa wa serikali ya Ufaransa amesema kwa vile sasa serikali ya Ujerumani tayari imeundwa ni muhimu kufanya juhudi hizo kwa pamoja.
Udukuzi ni nyeti Ujerumani
Suala la udukuzi wa serikali hususan ni nyeti nchini Ujerumani kutokana na upelelezi mkubwa wa raia uliofanyika wakati wa utawala wa Ukomunisti wa iliokuwa Ujerumani Mashariki na wakati wa utawala wa Hitler na ndio maana kukawa na ghadhabu kubwa baada ya mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Upelelezi la Marekani (NSA) Edward Snowden kufichuwa upelelezi uliokuwa ukifanywa na shirika hilo.
Merkel amesema hapo Jumamosi kwamba bila ya shaka inabidi wachukuwe hatua zaidi katika suala la ulinzi wa data barani Ulaya.Ujerumani hadi sasa imekuwa ikishinikiza bila ya mafanikio kuwepo kwa makubaliano ya kutopelelezana na serikali ya Marekani.
Katika ziara yake hiyo ya Ufaransa Merkel pia anapanga kujadili na Hollande mipango ya ushirikiano zaidi ya kuhifadhi mazingira kabla ya kufanyika kwa mkutano wa dunia wa mabadiliko ya tabia nchi nchini Ufaransa hapo mwakani halikadhalika sera za usalama na hususan kuhusiana na Afrika.
Mwandishi: Mohamed Dahman /Reuters/dpa
Mhariri:Hamidou Oummilkheir