Merkel asema yuko tayari kuongoza muungano wa 'Jamaica'
7 Oktoba 2017Merkel alishinda muhula mwingine katika uchaguzi wa Septemba 24 lakini chama cha mrengo mkali wa kulia cha Alternative für Deutschland - Chama Mbadala kwa Ujerumani (AfD), kiliwinda kura milioni moja kutoka muungano wake wa vyama vya kihafidhina, na hivyo kumuacha bila uwezekano wa kuwa na muungano wa dhahiri kuongoza taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya.
Tayari Merkel amesema atafanya mazungumzo ya awali kuhusu kuunda ushirikiano kati ya muungano wake wa vyama vya Chrisitin Democratic Union (CDU), na Christian Social Union (CSU) pamoja na vyama vidogo viwili, chama kinachoegemea biashara cha Free Democrats (FDP), na chama cha watetezi wa mazingira cha Kijani (Die Gruen).
Merkel alisema katika hotuba aliyoitoa katika mji wa mashariki mwa Ujerumani wa Dresden siku ya Jumamosi kwamba majadiliano yatakuwa "magumu", lakini akaongeza kuwa: "Natumai muungano utawezekana kuundwa."
Muungano wa kihistoria
Muungano kama huo - ambao utakuwa wa kwanza nchini Ujerumani kwa ngazi ya taifa -- umepewa jina la "Muungano wa Jamaica" kwa sababu rangi za bendera za vyama hivyo vitatu zinaendana na rangi nyeusi, njano na kijani za bedera ya taifa hilo la kanda ya Caribbean.
Mazungumzo hayo huenda yakaanza kwa ari katika siku chache zijazo lakini uundwaji wa serikali hautarajiwi kabla ya mwisho wa mwaka huu wa 2017. Siku ya Jumapili, Merkel na viongozi wa chama chake cha CDU wanatarajiwa kukutana mjini Berlin pamoja na washirika wao wa Bavaria, chama cha CSU, kukubaliana juu ya mpango wa pamoja kwa ajili ya miaka minne ijayo.
Muungano wa CDU/CSU ulishinda asilimia 33 ya kura katika uchaguzi wa Septemba, matokeo mabaya zaidi tangu mwaka 1949, huku chama cha Social Democratic ambacho ndiyo mshirika mdogo katika serikali ya sasa ya muungano mkuu, kiligaragazwa kwa kupata asilimia 20 tu ya kura.
"Ni dhahiri kwamba katika siku za usoni, chama cha Social Democrat SPD hakiwezi kutawala kwa ngazi ya taifa," alisema Merkel.
Hata hivyo uchaguzi huo ulikiingiza bungeni kwa amara ya kwanza chama kinachopinga Uislamu na uhamiaji cha AfD, kilichopata asilimia 12.6 ya kura, huku chama cha FDP kikipata asilimia 10.7 na kile cha Kijani kikipata asilimia 8.9.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri. Yusra Buwayhid.