Merkel ashinda uchaguzi kwa kishindo
22 Septemba 2013Matokeo ya kura za maoni baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa zilizofanywa na vituo vya televisheni, yanaonyesha muungano wa kihafidhina wa Merkel wa vyama vya Christian Democratic Union, CDU, na Christin Social Union, CSU, umeshinda asilimia 42.5, ambapo kama matokeo haya yatathibitishwa yatakuwa mazuri kabisa tangu mwaka 1990.
Matokeo haya yanawapa mahafidhina fursa ya kushinda wingi unaotakiwa bungeni kuweza kuunda serikali peke yao, ushindi ambao utakuwa wa kihistoria kwa Bi Merkel mwenye umri wa miaka 59, ambaye uongozi wake imara wakati wa mzozo wa sarafu ya euro umemfanya kuwa maarufu sana nyumbani Ujerumani. Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha ARD, Merkel ameshinda wingi unaotakiwa kuweza kuunda serikali bila kushirikiana na chama kingine.
"Ni matokeo mazuri sana," amesema Merkel, huku akitabasamu. "Kwa pamoja tutashirikiana tutafanya kila linalowezekana kuifanya miaka minne ijayo kuwa ya ufanisi kwa Ujerumani," Merkel aliwaambia wafuasi wa chama chake cha CDU waliokuwa wakishangilia mjini Berlin. "Uongozi wa chama utajadili kila kitu mara tu tutakapopata matokeo ya mwisho rasmi, lakini tunaweza kusherehekea usiku wa leo," akaongeza kusema Bi Merkel.
Hata hivyo ushirikiano wake na chama cha Free Democratic, FDP, uko mashakani huku chama hicho kinachopendelea wafanyabiashara kikiwa na asilimia 4.7, chini ya asilimia 5 inayohitajika kubakia kuwakilishwa bungeni. Wasiwasi huu unazidishwa na chama kipya cha "Mbadala kwa Ujerumani" - AfD, ambacho kimepata asilimia 4.9, chini ya kiwango kinachohitajika kuweza kuingia bungeni. Chama cha Social Democratic, SPD, kimepata kiasi asilimia 26. Chama cha wanamazingira, The Greens, kimepata asilimia 8 na chama cha Die Linke, asilimia 8.5.
Uwezekano wa kuunda serikali ya mseto
Iwapo Merkel hatapata wingi wa kutosha kuweza kuunda serikali, atalazimika kuanza mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto na cha chama cha SPD, alichoshirikiana nacho katika serikali yake ya kwanza kati ya mwaka 2005 na 2009. Mazungumzo hayo yumkini yakachukua miezi kadhaa na serikali mpya huenda ikakubali sera za mrengo wa shoto kama vile kiwango cha chini cha mshahara na kupandishiwa kodi wanaopata mishahara minono.
"Leo jioni hatutaahidi kujiunga katika mseto wowote," amesema Andrea Nahles, kiongozi wa chama cha SPD anayeshikilia nafasi ya pili ya uongozi wa chama hicho. Nahles ameyasema hayo akidokeza juu ya upinzani mkali ndani ya chama hicho kuhusu suala la kushirikiana na kansela Merkel kwa mara ya pili katika muongo mmoja.
Baadhi ya washirika wa Ujerumani barani Ulaya wana matumaini kwamba chama cha SPD kitamshinikiza kansela Merkel alegeze msimamo wake kuhusu mataifa yanayoyumba kiuchumi katika kanda inayotumia sarafu ya euro kama vile Ugiriki, lakini uwezekano wa kufanyika mageuzi makubwa ya sera ni mdogo.
Merkel, mtoto wa kike wa mchungaji wa kanisa la Kiprotestanti aliyekulia eneo la Ujerumani Mashariki, sasa anaelekea kuwa kansela wa tatu kushinda chaguzi tatu tangu kumalizika vita vikuu vya pili vya dunia mwaka 1945. Mshauri wake, Helmut Kohl, na Konrad Adenauer, pia walishinda chaguzi tatu.
Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/DPA
Mhariri: Mohammed Abdulrahman