Merkel azuru India
29 Oktoba 2007Kansela Angela Merkel ataandamana na wajumbe 30 wakiwemo mkurugenzi mpya wa kampuni ya Siemens, Peter Loescher na mameneja wa ngazi za juu wa kampuni ya kemikali ya BASF na shirika la usfiri wa treni la Ujerumani Deutsche Bahn.
Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya India, Navtej Sarna, ameesema India na Ujerumani zitasaini mikataba kuhusu ushirikiano katika maswala ya ulinzi, sayansi na teknolojia na haki miliki. Hata hivyo msemaji huyo hakutoa maelezo zaidi.
Ziara ya kansela Merkel nchini India itakuwa ya kwanza tangu alipochukua hatamu ya uongozi. Kwa muda mrefu Ujerumani imekuwa ikiyashughulikia sana maswala ya China na tayari kansela Merkel amewahi kuitembelea China mara mbili. Lakini kwa kuwa India inainukia kwa kasi kiuchumi na ina maono makubwa Bi Merkel amesema kuna haja ya Ujerumani kutafuta ushirikiano na India.
´Naamini sisi kama Wazungu tuna nafasi zote katika nchi kama India. Tunachotakiwa kufanya ni kujishughulisha na tuchukue hatua kwa haraka.´
Kansela Merkel anatarajiwa kukutana na waziri mkuu wa India Manmohan Singh hapo kesho mjini New Delhi. Mazungumzo yao yatatuwama juu ya kujenga ushirikiano wa kibiashara. Waziri mkuu Manmohan Singh ameahidi leo kwamba ataendelea kufuatilia sera ya biashara huru. Aidha kiongozi huyo amesema India itaendeleza kasi ya ukuaji wa kiuchumi katika kipindi kirefu kijacho.
India inachukua nafasi ya tatu katika orodha ya nchi zilizoendelea zaidi kiuchumi barani Asia. China inaongoza katika orodha hiyo ikufuatiwa na Japan. Lakini sio wote wanaofaidi kutokana na kunawiri kwa uchumi nchini India kama anavyosema Sanjay Gupta.
´Nadhani sio kila mtu nchini India anayenufaika kutokana na ukuaji wa kiuchumi kwa mfano wakulima. Ni jambo la kushangaza ni wangapi wanaohitaji msaada. Unaposafiri katika maeneo ya mashambani utaona watu maskini hohehahe ambao hawajui maisha yao yatakuwaje kesho.´
Kwa mujibu wa takwimu rasmi za wizara ya kazi nchini India idadi ya jamii zinazokabiliwa na umaskini uliokithiri nchini humo imepungua tangu mwaka wa 2000. Hata hivyo kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni wakaazi milioni 800 nchini India bado wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.
Maswala mengine yanayotarajiwa kujadaliwa wakati wa ziara ya kansela Merkel nchini India ni mabadiliko ya hali ya hewa na ushirikiano wa karibu kati ya nchi zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani, G8 na nchi zinazoinukia kiuchumi duniani kama vile India. Ujerumani hivi sasa inashikilia uenyekiti wa nchi za G8.