Merkel: Chuki dhidi ya Wayahudi ikabiliwe
10 Oktoba 2019Hayo Kansela Merkel ameyasema Alhamis katika mkutano wa vyama vya wafanyakazi mjini Nuremberg, siku moja baada ya mshambuliaji mwenye sera za unazi-mamboleo kuwauwa watu wawili, akilenga sinagogi la Wayahudi katika mji wa Halle mashariki mwa Ujerumani.
Katika hotuba yake Kansela Angela Merkel ameeleza kuwa kama mamilioni ya Wajerumani wengine alishtushwa na kufadhaishwa na shambulizi la jana Jumatano, akisema, kila mmoja anafahamu kwamba kulikuwepo uwezekano wa watu wengi sana kuuawa.
Wito kwa taasisi zote kupinga chuki na ubaguzi
Katika shambulio hilo mjini Halle, kijana Mjerumani aliyetambulishwa kwa jina la Stephan B alijaribu lakini akashindwa kuingia katika sinagogi la Wayahudi, walipokuwa wakiadhimisha siku kuu ya kidini ya Yom Kippur. Baadaye aliwauwa kwa bunduki mwanamke mpita njia na mwanamme aliyekuwa katika mkahawa wa kituruki.
Bi Merkel amezitolea wito taasisi zote kushirikiana katika kupinga itikadi ya chuki nchini Ujerumani. ''Tunafurahia kila sinagogi, na kila jamii ya Wayahudi na maisha ya Wayahudi wote katika nchi yetu. Hiyo ina maana kwamba wawakilishi wa serikali wanapaswa kutumia kila nyenzo ya dola kupambana na chuki, ghasia na uhasama dhidi ya watu wengine.'' Amesema Merkel.
Chanzo cha habari cha kijeshi kimearifu kuwa mshambuliaji aliyetambuishwa kama Stephan B. alipata mafunzo ya jeshi. Jina lake la pili halitajwi katika vyombo vya habari kulingana na sheria za Ujerumani.
Steinmeier aiita siku ya aibu
Awali leo, rais wa shirikisho la Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ametembelea sinagogi lililoshambuliwa, akasema ilikuwa siku ya aibu, kuona shambulizi hilo likitokea katika nchi ya Ujerumani, historia yake ikitiliwa maanani.
Steinmeier amesema anao uhakika kwamba Wajerumani walio wengi wanauchukulia uyahudi kama sehemu ya maisha ya nchi yao, na kuhimiza kila mmoja kuchangia katika kuhakikisha usalama wa Wayahudi.
Mkuu wa baraza la wayahudi nchini Ujerumani Josef Schuster ameikosoa polisi ya Ujerumani kwa kushindwa kuweka ulinzi nje ya sinagogi lililoshambuliwa, wakati waumini wa kiyahudi walipokuwa ndani wakisali. Kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara yenye misingi ya chuki dhidi ya Wayahudi, taasisi nyingi za jamii hiyo huwa zikipatiwa ulinzi wa kudumu katika miji mikubwa.
Hata hivyo, mkuu wa umoja wa maafisa wa polisi nchini Ujerumani Oliver Malchow amelitetea jeshi hilo, akisema haelewi ikiwa wanalazimika kuweka ulinzi wa kudumu kuzunguka kila nyumba ya ibada nchini Ujerumani.
Mshambuliaji Stephan B alikamatwa jana na kuwekwa kizuizini, na ofisi ya mwendeshamashtaka mkuu wa shirikisho la Ujerumani ameiomba idara ya mahakama kutoa haraka kibali cha kumkamata rasmi ili afikishwe kizimbani.
rtre, dpae