Merkel kuanza majadiliano ya kuunda serikali
23 Septemba 2013Baada ya kampeni ambayo ilituwama zaidi katika haiba ya Merkel , akiwa mpole, mwenye kutambua mambo na akiyahakikishia mataifa ya eneo la euro kuhusu kutuliza mzozo wa madeni, amekiongoza chama chake cha Christian Democratic Union , CDU na kupata ushindi ambao ni wa kwanza wa karibu ya kupata wingi wa kutosha kuweza kutawala peke yake katika muda wa nusu karne.
Nchi ya Merkel
"Jamhuri ya Merkel", limeandika gazeti la Spiegel katika maoni yake ya mhariri, ambao umesema kuwa baada ya ushindi wa kishindo ambao umempatia kansela kipindi cha tatu, "Ujerumani hatimaye imekuwa nchi ya Angela Merkel".
Kama anavyopenda kufanya shughuli zake, Merkel ameahidi kuwa "tutatumia matokeo hayo kwa kuwajibika na kwa uangalifu," lakini amesisitiza kuwa anania ya kutumikia kipindi chake hadi mwaka 2017, wakati wafuasi wake waliojawa na furaha wakipiga kelele , "Angie, Angie , Angie".
Chama cha CDU na washirika wake wa jimbo la Bavaria wamewasambaratisha mahasimu wao wa siasa za wastani za mrengo wa shoto kwa kile Merkel alichokiita , "matokeo mazuri mno" ya asilimia 41.5, yakiwa matokeo yao mazuri kabisa katika miaka 23.
Mshirika akwaa kisiki
Hata hivyo , kuporomoka kwa kushutua kwa chama kidogo mshirika wa Merkel katika serikali chama cha FDP baada ya zaidi ya nusu karne kuwamo katika bunge kuna maana kwamba sasa analazimika kuangalia washirika wengine wa kuunda muungano.
Chama kinachoonekana kuwa na uwezekano wa kuunda muungano huo ni chama cha siasa za wastani za mrengo wa shoto cha Social Democratic, SPD , ambacho kimepata chini ya asilimia 26 ya kura. Mgombea wake Peer Steinbrück amesema jana jumapili(22.09.2013) kuwa " mpira sasa uko upande wa Merkel. "Anapaswa kutafuta wingi katika bunge."
Uwezekano mwingine ambao una shaka unaweza kuwa muungano wa Merkel na walinzi wa mazingira chama cha kijani, ambao wamepata asilimia 8.4 ya kura, licha ya kuwa vyama vyote hivyo viwili katika kampeni viliondoa uwezekano kama huo wa muungano kutokana na tofauti zao kubwa za sera na chama cha Merkel cha CDU.
Kwa tahadhari na kama kawaida akijilinda , Merkel amesema kuwa atasubiri hadi mwisho wa hesabu ya kura na kupata matokeo kamili na kisha ndipo atakapoanza na hatua ya kwanza, hatua kwa hatua.
Hara haraka
"Hatutaanza mchezo wa kubahatisha, amesema, akitumia msemo wa kamari ambao una maana ya kukurupuka na kufanya mambo bila tahadhari.
Merkel binafsi amesema kuwa, baada ya vyama vingine kuwa vimejeruhiwa katika muungano wa hapo kabla pamoja nae, "huenda hawatapata mtu yeyote ambaye yuko tayari kufanya muungano nae".
Kwa hali yoyote, wachunguzi wanatarajia siku ama wiki kadha za majadiliano kuhusu sera na nyadhifa za uwaziri kati ya washirika wanaotaka kuunda serikali pamoja na Merkel.
Sura yoyote itakayojitokeza ya serikali mpya, athari katika eneo la euro pamoja na duniani kwa jumla zinaonekana na wadadisi kuwa ni ndogo .
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Iddi Ssessanga