1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Putin wajadili mizozo ya Ukraine na Syria

19 Agosti 2018

Rais wa Urusi Vladimir Putin na kansela wa Ujerumani Angela Merkel wamejadiliana kuhusu mizozo nchini Ukraine na Syria, pamoja na Iran na mradi wa bomba la gesi ambao umekumbana na upinzani kutoka Marekani.

https://p.dw.com/p/33NTN
Deutschland Treffen Angela Merkel Wladimir Putin auf Schloss Meseberg
Picha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

Haya yamefanyika wakati  wa  mazungumzo mazito  nje  ya  mji  wa  Berlin ambayo  yalimalizika bila  kupigwa hatua  maalum.

Msemaji  wa  serikali  ya  Urusi Dmitry Peskov  amewaambia waandishi  habari  hakuna  maendeleo  yaliyofikiwa, lakini mkutano huo ulikuwa  tu  una  lengo  la "kuangalia  vipimo"  baada  ya mkutano  wa  Merkel  na  Putin katika mji  wa  kitalii  ulioko  katika bahari  nyeusi  wa  Sochi mwezi  Mei.

Mahusiano  baina  ya  nchi  hizo  mbili yamedhoofika tangu  pale Urusi  ilipolinyakua  kwa  nguvu  jimbo  la  Crimea  la  Ukraine mwaka  2014.

Viongozi  hao  wawili  wote wanauangalia  mradi  wa  bomba  la  gesi unaojulikana  kama  Nord Stream 2, kuwa  ni mradi  wa  kibiashara zaidi, licha  ya  mashambulio  ya  mara  kwa  mara  kutoka  Marekani ,na  serikali  za  Ukraine, Peskov  alisema.

Merkel alisisitiza matarajio yake

"Hii  ndio  sababu  ni  muhimu kuchukua  hatua  dhidi  ya  uwezekano wa  mashambulizi ambayo  si  ya  ushindani  na  kinyume  na  sheria kutoka  katika  nchi  ya  tatu ili kuweza  kukamilisha  mradi  huu hatimaye," aliwaambia  waandishi  habari  muda  mfupi  kabla  ya Putin kurejea  nyumbani  nchini  Urusi. Haikufahamika  mara  moja ni "hatua"  gani  zinaweza  kuhusika.

Deutschland Treffen Angela Merkel Wladimir Putin auf Schloss Meseberg
Kansela Angela Merkel na Rais Vladimir PutinPicha: Reuters/A. Schmidt

Mwanzoni  mwa  mazungumzo  hayo, Merkel  alisisitiza  matarajio yake  kwamba  Ukraine  inapaswa  kuendelea  kuwa  na  jukumu kama  nchi  inayopitia  gesi  katika  Ulaya, na  kukaribisha  mwanzo wa  majadiliano  miongoni  mwa Umoja  wa  Ulaya, Ukraine  na  Urusi kuhusiana  na  suala  hilo.

Putin, akizungumza  katika  kasri  la  serikali  ya  Ujerumani  la Meseburg, alisema  hatua  kama  hizo zinapaswa  kueleweka  kwa mtazamo  wa  kibiashara.

"Suala  kuu ni  kwamba nchi  ya  Ukraine  kama  sehemu  ya  kupitia, ambayo  ni  ya  asili  kwetu, inatimiza mahitaji  ya  kiuchumi" alisema. "Nord Stream 2 ni  mradi  wa  kiuchumi  tu."

Marekani inaibinya  Ujerumani  kusitisha  bomba  hilo  ambalo linasafirisha  gesi  kutoka  Urusi  chini  ya  bahari  ya  Baltic, ikidai kuwa  itaongeza  utegemezi  wa  Ujerumani  kwa  Urusi kwa  ajili  ya nishati.

Ukraine  inahofia kwamba  bomba  hilo litaruhusu Urusi kuitenga katika  biashara  ya  kuwa  nchi  inayopitia  gesi, wakati  majirani  wa Ujerumani  upande  wa  Mashariki  mwa  Ulaya  waan  hofu  juu  ya hatua  za  Urusi  kuziingilia.

Peskov amesema  kitisho  hicho  cha  uwezekano wa  vikwazo  vya Marekani dhidi  ya  makampuni  yanayohusika  katika  mradi  huo hakikujadiliwa  katika  mkutano  wa  hapo  jana  Jumamosi.

Ni muhimu kuepusha mzozo wa kibinadamu Idlib

Akisimama  pamoja  na  Putin kabla  ya  mazungumzo  hayo, Merkel alisema  nchi  hizo  mbili,  lakini  hususan  Urusi  kama  mwanachama wa  kudumu  wa  baraza  la  Usalama  la  Umoja  wa  mataifa , ina jukumu  la  kujaribu  kutatua  mapigano  yanayoendelea  nchini Ukraine  na  Syria.

Deutschland Treffen Angela Merkel Wladimir Putin auf Schloss Meseberg
Viongozi wa Urusi na Ujerumani wakizungumza na waandishi wa habariPicha: Reuters/A. Schmidt

Amesema  anapanga  pia  kuzusha  masuala ambayo  yanaonekana kuwa  vikwazo ya  haki  za  binadamu kwa  Putin, na  kujadili mahusiano  ya  pande  mbili.

"Nina  maoni  kwamba  masuala  yenye  utata yanaweza  tu kutatuliwa  kupitia  majadiliano na  katika  majadiliano,"  amesema.

Merkel amesema  ni  muhimu  kuepusha  mzozo  wa  kibinadamu katika  jimbo  la  Idlib, Syria  pamoja  na  majimbo  ya  karibu, na kusema  yeye  pamoja  na  Putin tayari  wamelijadili  suala  la mabadiliko  ya  katiba  pamoja  na  uwezekano  wa  uchaguzi  wakati walipokutana  mjini  Sochi  mwezi Mei  mwaka  huu.

Putin aewaambia  waandishi  habari  kwamba kila  kitu  ni  lazima kifanyike  kuwasaidia  wakimbizi  wa  Syria  kurejea  katika  nchi  yao na  kwamba  Syria  inahitaji  msaada  wa  kuijenga  upya. Viongozi hao  wawili hawakujibu  maswali  ya  waandishi  habari.

Kuhusu  Ukraine, Merkel  alisema ana  matumaini  kwamba  juhudi mpya  zinaweza  kuchukuliwa  mwanzoni  mwa  mwaka  mpya  wa masomo kutenganisha  majeshi  ya  Ukraine  na  yale  wanaotaka kujitenga  katika  maeneo  ya  mstari  wa  mbele  katika  jimbo  la Donbass.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri: Jacob Safari