Merkel: Sina njia mbadala kuhusu mzozo wa wahamiaji
29 Februari 2016Akizungumza jana wakati wa mahojiano na kituo cha televisheni cha Ujerumani, ARD, Merkel amesema sera ya kufungua mipaka kwa wahamiaji bado itaendelea na ametupilia mbali suala la kuwepo kiwango maalum kwa wakimbizi wanaoingia, akisema hakuna uhakika wa kuamini kwamba tatizo hilo linaweza kutatuliwa kwa kila nchi kuifunga mipaka yake.
''Nadhani yeyote anayeiangalia Ujerumani, anapaswa pia kuiangalia Ulaya na kuvuka mipaka ya Ulaya. Maadili yetu ndiyo yanaifanya Ujerumani kuwa kivutio machoni mwa wakimbizi wengi. Ndiyo maana wanakuja hapa. Tungependa kufanikiwa kwa pamoja kusimamia kila kitu, ikiwemo idadi ya namba ya wakimbizi wanaoingia,'' alisema Merkel.
Merkel amesema hana mpango mbadala na anaamini kwamba yuko katika njia sahihi kwenye juhudi za kugawana wakimbizi ndani ya Ulaya, huku akielezea matatizo yanayosababisha watu kukimbia. Kansela huyo amekiri kwamba ana wasiwasi kuhusu migogoro ya wahamiaji ndani ya Umoja wa Ulaya na amesisitiza haja ya kulizuia bara la Ulaya lisifarakane, akisema utengamano wa wahamiaji ni muhimu.
Aidha, Merkel amekemea vitendo vilivyofanywa na waandamanaji wanaowapinga wahamiaji Februari 18, katika jimbo la Saxony, akiviita ''visivyokubalika.'' Amesema hatua ya kukabiliana na mzozo wa wahamiaji imekuwa ngumu, lakini hiyo inadhihirisha sifa ya Ujerumani katika dunia na kwamba huu ni wakati muhimu sana kwa historia ya nchi.
Wahamiaji waleta upinzani katika serikali ya muungano
Suala la wahamiaji halijaigawa tu Ulaya, bali kuna upinzani mkubwa hata ndani ya Ujerumani na kwenye serikali ya muungano. Wanasiasa kutoka jimbo la Bavaria wa chama cha Christian Social Union-CSU, chama ndugu na chama cha Merkel cha Christian Democratic Union-CDU, wamekosoa msimamo wa kansela huyo na wanataka kuwepo na kiwango cha idadi ya wahamiaji wanaoingia nchini Ujerumani kama ilivyo nchini Austria.
Chama cha Merkel kinakabiliwa na uchaguzi wa wabunge Machi 13 katika majimbo matatu kati ya 16 nchini Ujerumani. Huo utakuwa uchaguzi wa kwanza kufanyika tangu ulipoanza mzozo wa wakimbizi.
Katika hatua nyingine, Merkel amesema Umoja wa Ulaya hauwezi kuacha Ugiriki katika hali ya sintofahamu dhidi ya kuongezeka kwa wakimbizi, kutokana na kufunga mipaka. Katika mahojiano hayo na Anne Will, Merkel amesema hawawezi kuitenga Ugiriki na kwamba nchi hiyo haiko ndani ya eneo linalotumia sarafu ya Euro kwa lengo la kutumbukia kwenye mizozo. Amesema makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi yake na Uturuki yanahitaji kutekelezwa ili kuzuia iwmbi la wakimbizi wanaoingia Ulaya.
Akizungumzia visa vya udhalilishaji wanawake kingono wakati wa mkesha wa Mwaka Mpya mjini Cologne, Merkel amesema sheria zinapaswa kuwa wazi tangu mwanzo kwa wakimbizi, akiongeza kuwa utengamano sio suala la hiari, bali ni jambo la lazima.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA,AFP,RTRE, ARD,http://bit.ly/1oRXLA1
Mhariri:Iddi Ssessanga