1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel yuko Uturuki kujadili wakimbizi

Admin.WagnerD8 Februari 2016

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani yuko Uturuki ambapo anakutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Ahmet Davutoglu na baadae Rais Tayyip Recep Erdogan kwa mazungumzo juu ya kupunguza wimbi la wakimbizi wanaokimbilia Ulaya.

https://p.dw.com/p/1HrNJ
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akikaguwa gwaride la heshima na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davotoglu wakati alipowasili Ankara. (08.02.2016)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akikaguwa gwaride la heshima na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davotoglu wakati alipowasili Ankara. (08.02.2016)Picha: Reuters/U. Bektas

Merkel anafanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu na baadae kukutana na Rais Recep Tayyip Erdogan katika mji mkuu wa Ankara wakitarajia kupata ufumbuzi wa kupunguza miminiko wa wakimbizi wanaokimbilia Ulaya.

Uturuki nchi muhimu inayotumiwa na wahamiaji kuingilia Ulaya ni suala kuu katika juhudi za kidiplomasia za Merkel kupunguza wimbi la wakimbizi barani Ulaya.

Mazunguzo yake na viongozi wa serikali ya Uturuki yanakuja wakati Uturuki ikikabiliwa na ongezeko la shinikizo kufunguwa mpaka wake kwa wakimbizi 35,000 wa Syria ambao wamekusanyika mpakani wakiyakimbia mashambulizi yanayofanywa na vikosi vya serikali.

Uturuki tayari imewapa hifadhi wakimbizi wa Syria milioni 2.5 na imesema uwezo wake wa kupokea wakimbizi umefikia kikomo lakini imedokeza kwamba itaendelea kutowa msaada kwa wakimbizi hao.

Merkel aunga mkono msaada kwa Uturuki

Merkel ameunga mkono kwa nguvu makubaliano ya mwaka jana na Uturuki ambapo Uturuki itapatiwa msaada wa euro bilioni 3 ili nchi hiyo isaidie Ulaya kulinda mipaka yake.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akikaribishwa Ankara na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davotoglu (08.02.2016)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akikaribishwa Ankara na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davotoglu (08.02.2016)Picha: Reuters/U. Bektas

Makubaliano hayo yaliyosainiwa mwezi wa Novemba mwaka 2015 msaada wake unakusudia kugharamia matunzo ya wakimbizi milioni mbili na nusu ambao tayari wako nchini Uturuki.Lakini wiki iliopita pekee maelfu ya wakimbizi wapya kutoka Syria wamewasili mpakani mwa Uturuki wakikimbilia kunusuru maisha yao kufuatia mashambulizi ya serikali ikisaidiwa na mashambulizi ya anga ya Urusi katika mji wa Allepo.

Uturuki imeahidi kuwasaidia wakimbizi hao wakiwemo wanawake na watoto wengi ambao wamekwama mpakani lakini haikufunguwa mipaka yake na mashirika ya misaada yameonya kwamba wanakabiliwa na hali mbaya sana wakati wakisubiri msaada.

Wakimbizi kutotelekezwa

Naibu waziri mkuu wa Uturuki Numan Kurtulmus amekiambia kituo cha televisheni cha CNN nchini Uturuki kwamba nchi hiyo imefikia kikomo cha kupokea wakimbizi lakini hatimae watu hao hawana pa kukimbilia aidha itabidi wauwawe kutokana na mashambulizi ya mabomu au venginevyo wawafungulie mipaka.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.Picha: Getty Images/AFP/A. Altan

Ameongeza kusema kwamba hawako katika nafasi ya kuwaambia wasende kwani kwa kufanya hivyo itakuwa sana na kuwatelekeza katika mauti.

Rais Tayyip Recep Erdogan amesema Uturuki iko katika kitisho na kuahidi kwamba iwapo ikibidi watawaachilia wakimbizi hao aliowaita ndugu zao waiigie nchini Uturuki.

Msaada zaidi wahitajika

Uongozi wa Uturuki tayari umetangaza kwamba msaada wa fedha wa Umoja wa Ulaya kuisaidia nchi hiyo kuwadhibiti wakimbizi wasiingie Ulaya hautoshi.

Wakimbzi wa Syria walioko mpakani mwa Uturuki.
Wakimbzi wa Syria walioko mpakani mwa Uturuki.Picha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Haiko wazi iwapo suala la nchi hiyo kupatiwa msaada zaidi litajitokeza katika mkutano wa Merkel leo hii na viongozi wa Uturuki.

Maelfu ya wakimbizi waliingia Ulaya kupitia Uturuki mwaka jana Ujerumani ikipokea zaidi ya wahamiaji milioni 1.1 wanaotafuta hifadhi kwa mwaka 2015 pekee.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP /Reuters

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman