1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Messi aweka historia katika klabu ya Barca

17 Machi 2014

Mshindi mara nne wa tuzo ya mchezaji bora ulimwenguni Lionel Messi ameyaangazia macho mchuano wa wikendi ijayo dhidi ya Real Madrid, baada ya kuisaidia Barcelona kuisambaratisha Osasuna 7 - 0

https://p.dw.com/p/1BR1g
FC Barcelona - AC Milan
Picha: Lluis Gene/AFP/Getty Images

Messi alimpiku Paulino Alcantara na kuwa mfungaji wa magoli mengi katika historia ya klabu ya Barcelona. Messi alifunga mabao matatu jana na kufikisha 371 idadi ya magoli yake katika klabu ya Barca. Real Madrid wanaongoza ligi wakiwa na pengo la pointi nne dhidi ya Barca…miamba hao wawili watakutana Jumapili katika mchuano wa kukata na shoka wa El classico uwanjani Santiago Bernabeu.

Farasi wanne Uingereza?

Kinyang'anyiro cha English Premier League kinaendelea kupamba moto. Mambo yanaonekana kuwa ni mbio za farasi wanne baada ya Liverpool na Arsenal kusajili ushindi dhidi ya mahasimu wao wa jadi. Liverpool waliwakwaruza Manchester United mabao matatu kwa sifuri wakati nao Arsenal wakiponyoka na ushindi wa goli moja kwa sifuri nyumbani kwa Tottenham. Hivyo Arsenal, Liverpool na City zilichukua fursa ya kupunguza pengo baina yao na viongozi Chelsea ambao walijikwaa nyumbani kwa Aston Villa kwa kurambishwa goli moja kwa sifuri.

Champions league

David Moyes na vijana wake wa Manchester United wanaendelea kukosa usingizi kutokana na jinamizi linalowaandama..na mambo huenda yakawa mabaya hata zaidi wakati watakaporejea katika jukwaa la Ulaya Jumatano hii. Lazima Man Utd wageuze kichapo walichopata cha mabao mawili nyumbani kwa mabingwa wa Ugiriki Olympiakos katika Champions League. Zamani, Manchester ilifahamika kwa kuyabadilisha matokeo ya aina hiyo lakini kikosi cha sasa ni kama kivuli tu cha timu iliyokuwa ikitawala chini ya mkufunzi Sir Alex Ferguson.

Mabingwa wa Ugiriki Olimpiakos Piraeus wanatarajiwa kuwatoa jasho Manchester United
Mabingwa wa Ugiriki Olimpiakos Piraeus wanatarajiwa kuwatoa jasho Manchester UnitedPicha: A.Messinis/AFP/GettyImages

Chelsea wako katika nafasi nzuri ya kusonga mbele baada ya kutoka sare ya goli moja kwa moja na Galatasaray katika mkondo wa kwanza. Sasa vijana hao wa Jose Mourinho watalenga kumaliza kibarua kesho Jumanne katika uwanja ambao utamkaribisha tena mshambuliaji wa zamani Didier Drogba.

Katika mechi nyingine Real Madrid na Borussia Dortmund zilipata ushindi mkubwa katika mikondo ya kwanza dhidi ya Schalke na Zenit St Petersburg. Madrid waliwakalifisha Schalke magoli sita kwa moja katika mkondo wa kwanza na kocha Carlo Ancelotti ana kila sababu ya kukifanyia kikosi chake mageuzi makubwa kama hatua ya kujiandaa kwa elclassico.

BVB waliwabwaga Zenit magoli manne kwa mawili ugenini lakini ni lazima Jurgen Klopp afahamu kuwa lolote linaweza kutokea kama watakuwa wazembe uwanjani..

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef