Messi aweka historia ya mabao 400 ya La Liga
14 Januari 2019Luis Suarez ambaye alifunga mabao mawili, alimuandalia pasi Messi kufunga bao hilo la kihistoria, ambalo lilipatikana katika mchuano wa 435 wa Muargentina huyo akiwa na Barca. Messi sasa amefikisha mabao 17 katika mechi 17 msimu huu. Kocha wake Ernesto Valverde alimmiminia sifa mshambuliaji huyo hatari "Nnafikiri atafunga mabao 500 katika ligi lakini mabao 400 ni kitu cha ajabu sana. Ni kitu rahisi kusema lakini hauwezi kujua ukweli wa hilo hadi pale unapojaribu kuyafunga mabao hayo. Ni mchezaji asiye wa kawaida kabisa. Sio mfungaji tu, alizaliwa kuwa mfungaji lakini pia anatengeneza mchezo, kuwaandalia wenzake pasi, anaipa timu kila kitu kwa ujumla.
Ilikuwa hatua kubwa sana kwa Messi, ambaye amekuwa mfungaji bora wa mabao katika ligi hiyo tangu mwaka wa 2014, huku Cristiano Ronaldo akiwa wa pili na mabao 311.
Barca wana pointi 43, tano mbele ya Atletico Madrid iko katika nafasi ya pili baada ya kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya Levante mapema jana, na kufikisha pointi 38 katika mechi 19. Sevilla wanakamata nafasi ya tatu na pointi 33 baada ya kupoteza 2-0 dhidi ya Athletic Bilbao.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga