1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Mfalme Afonso I wa Kongo aliyeshiriki biashara ya utumwa

Yusra Buwayhid
23 Desemba 2020

Afonso I wa Kongo alikuwa na uhusiano wa karibu na wenye maslahi na mkoloni Ureno. Mwanzoni, alishirikiana na Ureno katika biashara ya utumwa, lakini baadaye akaikataa kuhusika nayo unyanyasaji wa watumwa ulipokithiri.

https://p.dw.com/p/3n7ub

Mfalme Afonso I wa Kongo aliyeshiriki biashara ya utumwa

Afonso alizaliwa wapi? Afonso I wa Kongo, alizaliwa Mvemba a Nzinga mwaka 1456, na kumrithi baba yake ufalme João I wa Kongo. Alitawala Ufalme wa Kongo kuanzia 1507 hadi 1542.

Afonso anajulikana kwa lipi? Baba yake aliwakaribisha wasafiri wa kwanza wa Kireno waliowasili katika ufalme wake. Lakini Afonso aliuendeleza zaidi uhusiano huo kwa kuikubali dini ya Kikristo na kuwachana na maadili ya kitamaduni. Baadhi ya wanahistoria wanaliangalia hili kama mkakati wa kuhakikisha kunakuwako uhusiano mzuri na Ureno. Walakini, alikuwa muangalifu katika kutunza ushirikiano na Wareno uliokuwa na faida kwake na alionyesha ustadi wa mazungumzo kupitia barua zake nyingi ambazo alimwandikia Mfalme Manuel, haswa mara tu biashara ya watumwa ilipokithiri kwa manyanyaso.

African Roots | Afonso 4
Asili ya Afrika

Elimu ilimaanisha nini kwa Afonso I? Ukristo ulikuja pamoja na kusoma na kuandika, na kama mtawala, Afonso mara kwa mara aliandikiana barua na Ufalme wa Kireno, hususana kuhusu masuala ya kidini nay a kuitawala. Halikadhalika alipeleka mmoja wa watoto wake, Henrique Kinu a Mvemba, kupata mafunzo ya kidini na kuwa kuhani. Henrique aliishia kuteuliwa kama mmoja wa maaskofu wa kwanza wa kanisa Katoliki la Afrika mnamo 1518.

Kwa namna gani Afonso alijihusisha na biashara ya utumwa? Wengi wanamlaumu Afonso kw akuhusika na biashara ya utumwa. Biashara ya utumwa wakati huo ilikuwa halali. Hata katika jamii za Kiafrika, kulikuwako watumwa, wengi wao walikuwa mateka wa vita – lakini walikuwa na haki tofauti na wale waliosafirishwa kwa meli. Walikuwa bado wanatimiziwa haki zao za kibinadamu na hata wanaweza kuupata tena uhuru wao.Ufalme wa Kireno uliwaangalia watumwa kama rasilmali yao muhimu. Na Afonso alikubali kufanya nao biashara ya utumwa, bila ya kutambua athari za biashara hiyo. Alikubalia utumwa ili Wareno wamsaidie kuunda mfumo wa kiutawala ndani ya ufalme wake pamoja na kujenga taasisi mbalimbali za kidini.

Mfalme Afonso I wa Kongo aliyeshiriki biashara ya utumwa

Kweli Afonso alitafakari juu ya athari za utumwa kwa watu wake? Mashamba yalipoongezeka huko São Tomé yalihitaji idadi kubwa ya wafanyikazi, na hivyo haja ya watumwa iliongezeka, na mara baada ya hapo, biashara hiyo ilianza kupanuka bila ya kiasi. Afonso alijaribu kuidhibiti. Katika barua aliyomuandikia Mfalme Manuel I, alilalamika juu ya jinsi biashara hiyo inavyouangamiza ufalme wake na kwamba anataka isimamishwe. "Nchi yetu inapugua idadi ya watu kabisa, na haupaswi kukubaliana na hili", alisema, akisisitiza kwamba "tumeamua kwamba hakutakuwa na biashara yoyote ya watumwa katika Ufalme wala njia ya kuwasafirishia."

African Roots | Afonso 5
Asili ya Afrika

Biashara hiyo ilikithiri kutokana na tamaa ya wafanyabiashara wa Kireno pamoja na watu wa Afonso, ambao aliwaeleza katika barua hiyo kwamba wanashawishika kutokana na bidhaa zinazoletwa na wafanyabiashara hao wa Ureno.

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.

-----------------------------------------------