Mfumuko wa bei wasababisha wimbi la maandamano
27 Juni 2022Mfumuko wa bei umesababisha wimbi la maandamano na migomo ya wafanyakazi duniani kote. Wiki iliyopita pekee kulishuhudiwa maandamano yaliyoongozwa na wanasiasa wa upinzani katika nchi za Pakistan, maandamano ya wauguzi nchini Zimbabwe, na huko nchini Ubelgiji wafanyakazi walio wanachama wa vyama vya wafanyakazi, wafanyakazi katika sekta ya reli waligoma nchini Uingereza, na mamia marubani nchini Marekani na baadhi ya wafanyakazi wa mashirika ya ndege barani Ulaya waligoma. Waziri mkuu wa Sri Lanka ametangaza kuanguka kwa uchumi nchini mwake baada ya nchi hiyo kukumbwa na mtikisiko wa kisiasa kwa wiki kadhaa. Wanauchumi wanasema uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umeongeza mfumuko wa bei na kupandisha zaidi gharama za nishati, bei ya mbolea, nafaka na mafuta ya kupikia huku wakulima kutoka kwenye kanda muhimu za kilimo duniani wakihangaika kuuza mazao nje ya nchi .