1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo wa madereva wa malori kutoka Kenya waathiri biashara

Shisia Wasilwa4 Januari 2022

Biashara kwenye mpaka wa Kenya na Uganda imeathiriwa baada ya madereva wa malori kutoka Kenya kugoma kwa kupinga kufanyiwa vipimo vya Covid-19 kwa lazima.

https://p.dw.com/p/457AW
Afrika Grenzübergang Stau LKW Kenia Uganda
Picha: Brian Ongoro/picture alliance

Vipimo hivyo vinavyogharimu dola 30 ni sawa na shilingi 3,394 za Kenya na madereva wanahitaji kupimwa kila baada ya siku 14. Vipimo hivyo ni vya lazima licha ya madereva hao kuonyesha nyaraka za kuwa wameshapimwa na hawana virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, wanapotaka kuingia nchini Uganda.

Madereva hao wanadai kuwa vipimo hivyo ni njama za mamlaka ya Uganda za kuwatwalia fedha zao. Sasa, wameapa kutorejea kazini hadi mwafaka baina ya serikali za mataifa hayo upatikane. Mgomo huo unaingia siku ya nne leo Jumanne.

Mgomo huu unajiri chini ya mwaka mmoja baada ya mwingine kama huo kutokea mwaka uliopita ambapo maafisa wakuu wa mataifa hayo kuafikiana kuondoa vikwazo hivyo. Mgomo huo ulisababisha urefu wa kilomita 50 wa malori 4,500 yaliyounda msongamano  upande wa Kenya kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Soma pia: Tanzania kushughulikia adha za madereva kwenye mipaka

Wasiwasi wa wafanyabiashara

Uganda iliagiza bidhaa zenye kima cha dola milioni 674 nchini Kenya mwaka 2020.
Uganda iliagiza bidhaa zenye kima cha dola milioni 674 nchini Kenya mwaka 2020.Picha: Brian Ongoro/picture alliance

Iwapo mgomo huu hautasitishwa, huenda taswira kama hiyo ikashuhudiwa tena. Mamia ya madereva hao sasa wamekwama katika mpaka wa Busia-Malaba huku bidhaa ambazo zilikuwa zisafirishwe nchini Uganda zikihofiwa kuharibika.

Madereva hao sasa wanazitaka serikali za mataifa husika kuingilia kati na kuangazia kilio chao. Msongamano huo huenda pia ukachangia kuongezeka kwa visa vya virusi vipya vya Omicron kwa mujibu wa wataalamu wa matibabu, iwapo hatua za dharura za kutafuta suluhisho hazitapatikana kwa dharura.

Soma pia :Madereva wa kigeni mashakani Afrika Kusini 

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, Uganda iliagiza bidhaa zenye kima cha dola milioni 674 nchini Kenya mwaka 2020. Mamlaka za mataifa ya Kenya na Uganda hazijatoa tamko lao kuhusu mgomo huo unaoendelea kuchafua sio tu mazingira ya biashara lakini pia mahusiano ya mataifa hayo.