Mhanga wa ubakaji aunguzwa moto India
5 Desemba 2019Msichana huyo alivamiwa akiwa njia kuelekea mahakamani na kundi la wanaume wakiwemo wawili ambao ni miongoni mwa wanaotuhiumiwa walihusika kumbaka. Walimvuta kwenye eneo la uwanja lililoko karibu na kumteketeza moto. Msichana huyo mwenye miaka 23 kutoka jimbo la kaskazini mwa India la Uttar Pradesh anapigania uhai wake hivi sasa baada ya kuunguzwa na moto leo. Inaelezwa kwamba alivamiwa na kundi hilo la wanaume na kuteswa kabla ya kumwagiwa mafuta ya petroli na kutiwa moto.
Hivi sasa msichana huyo yuko hospitali akitibiwa majeraha mabaya ya moto na madaktari wanasema hali yake ni mbaya. Polisi wamewakamata wanaume watano wakiwemo wawili wanaotuhumiwa kumbaka msichana huyo wakihusishwa na shambulio hilo la kumteketeza msichana huyo.
Kisa cha kubakwa msichana huyu kilitokea mwezi Machi mwaka huu,alibakwa na wanaume watano na polisi wakawakamata watatu kati yao wakati wengine wawili hawakupatikana. Polisi ya India inasema mhanga huyo amepekwa hospitali katika mji wa Lucknow kwa ajili ya matibabu mazuri huku ikithibitisha kwamba awali msichana huyo alifungua kesi na mmoja wa watu wanaotuhumiwa katika kesi hiyo ni miongoni mwa waliokamatwa leo.
Ikumbukwe kwamba visa vya ubakaji nchini India sio vigeni na katika jimbo hilo la Uttar Pradesh hili sio tukio la kwanza. Katika wilaya ya Unnao katika jimbo hilo mnamo mwezi Julai msichana mwengine alibakwa na polisi walifungua uchunguzi wa mauaji dhidi ya mbunge mmoja kutoka chama tawala baada ya msichana huyo wa miaka 19 kugongwa na kujeruhiwa vibaya na gari.
Familia ya msichana hiyo ilidai kwamba inaamini tukio hilo lilipangwa na mbunge Kuldeep Sign Sengar kutoka chama cha waziri mkuu Narendra Modi Bharatiya Janata BJP. Wiki iliyopita msichana mwingine wa miaka 27 kutoka mji wa kusini wa Hyderabad nae alibakwa na kisha kuteketezwa kwa moto, kisa kilichoibua maandamano makubwa kote nchini India. Mcheza sinema wa zamani Jaya Bachan ambaye ni mbunge alitowa mwito wa kuanza kuchukuliwa hatua ya kuwatia moto wanaobaka.
Bachan aliliambia bunge la India kwamba licha ya mwito wake kuonekana hatua kali lakini alisema anaamini umefika wakati watu kuchukua hatua mikononi mwao na kuwaweka hadharani wabakaji na kuwatia moto. Kadhalika mashirika ya kiraia yamelaani tukio hilo la ukatili ya kuwabaka wasichana na kuuliwa huku maandamano yakifanyika nchi nzima.