1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 10 ya mauaji, mateso na wakimbizi Syria

15 Machi 2021

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vimetimiza miaka 10 tangu pale vikosi vya serikali vilipolilazimisha wimbi la maandamano ya amani ya raia wa kawaida kugeuka na kuwa mapambano ya silaha, mauaji na ukatili.

https://p.dw.com/p/3qdiL
BG Photos and testimonies from Syrian photographers | Ghaith Alsayed
Picha: Ghaith Alsayed/OCHA

Miaka kumi ya vita vya kumng'owa na hadi sasa Rais Bashar Al-Assad angalipo akiwa amefanikiwa kurejesha sehemu kubwa ya udhibiti wa nchi iliyobomolewa vibaya kwa vita. 

Kwa wengine, miaka kumi hii imepita kama mchezo, lakini kwa Wasyria kila siku moja ndani ya muongo huu mmoja ni kama mwaka mzima. Mmoja wao ni Ahmad Houli, mvulana wa miaka 15, ambaye amelazimika kuishi maisha ya kifukara kwa kuokotaokota majalalani baada ya kupoteza nyumba yao katika mji wa Homs uliposhambuliwa. 

"Watu wenye silaha waliivamia nyumba yetu, nasi tukaogopa. Tulitupwa kwenye gari ya jeshi la Syria na kisha tukabwagwa kwenye eneo tusilolijuwa. Tuliishi kwenye mahema muda wote huo na miaka minne tu iliyopita ndiyo tumerejea Homs," anasema mvulana huyo akiwa kwenye vifusi vya majengo yaliyobomolewa kwa makombora kusaka chochote kinachoweza kumsaidia.

Takribani watu 400,000 wameshauawa

BG Photos and testimonies from Syrian photographers | Abood Hamam
Miaka 10 ya vita imeigeuza Syria kuwa uwanja wa magofu na vifusi.Picha: Abood Hamam/OCHA

Kwa mujibu wa Shirika la Kufuatilia Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza, idadi kamili ya watu waliopoteza maisha yao kwenye vita hivyo ni 388,652 kufikia tarehe juzi tarehe 13 Machi 2021, wengi katika hao wakiwa raia wa kawaida, ambao ni 117,368 na ambapo zaidi ya 22,000 kati yao ni watoto wadogo. 

Mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vya serikali ya Syria na makundi ya wanamgambo yanayoiunga mkono ndiyo yaliyoangamiza maisha ya watu wengi zaidi.

Kwa ujumla, tangu mwaka 2020 mapigano makali yamepunguwa kufuatia mkataba wa kusitisha vita kwenye eneo kaskazini magharibi mwa Syria na pia kutokana na watu kuelekeza vita vyao kwenye janga la virusi vya corona.

Shirika hilo pia limesajili kwa uchache vifo 16,000 kwenye magereza na mahabusu ya serikali tangu mzozo ulipoanza mwaka 2011, baada ya ukandamizaji wa kikatili uliofanywa na serikali dhidi ya maandamano ya amani.

Hata hivyo, lilisema idadi kamili ya vifo inaweza kuwa kubwa zaidi kwa sababu hisabu yake haikujumuisha watu wengine 88,000 wanaoaminika kufa wakiwa kwenye jela za serikali na wengine 200,000 ambao hawajulikani walipo hadi sasa.

Assad arejesha udhibiti wa nchi

Syrien Bashar Al-Assad 1999
Bashar Al-Assad ameweza kuhimili mapigano ya miaka 10 kwa msaada wa Urusi na Iran.Picha: Getty Images/AFP/R. Moghrabi

Kwa sasa, serikali ya Rais Bashar al-Assad inadhibiti zaidi ya asilimia 60 ya nchi baada ya mafanikio makubwa ya kijeshi yaliyochangiwa na msaada wa kijeshi kutoka Urusi na Iran dhidi ya wanamgambo wa makundi ya siasa kali na waasi wa kawaida ulioanza mwaka 2015.

Miongoni mwa maeneo ambayo bado hayajarejea mikononi mwa serikali ni pamoja na ngome ya mwisho kabisa ya waasi ya Idlib iliyo kaskazini magharibi, maeneo yanayoshikiliwa na Uturuki kwenye mpaka wa kaskazini, na yale ya kaskazini mashariki ambayo yanashikiliwa na waasi wa Kikurdi wanaoungwa mkono na Marekani. 

Vita hivi vya miaka kumi vimewalazimisha zaidi ya nusu ya raia milioni 17 wa nchi hiyo kuyakimbia makaazi yao na kusaka hifadhi kwengineko duniani, wengi wao kwenye mataifa jirani, hasa Uturuki.