Miaka 100 ya benki kuu ya Marekani
23 Desemba 2013Kwa miaka 100 sasa, benki kuu ya Marekani imekuwa ikisimamia sarafu ya nchi hiyo Dola, ambayo ndiyo sarafu maarufu zaidi duniani. Benki hiyo ilianzishwa Disemba 23 mwaka 1913 baada ya kutungwa kwa sheria yake kufuatia migogoro kadhaa ya kifedha, na hasa ule uliofahamika kama 'hofu kuu' mwaka 1907.
Sheria ya benki kuu ya Marekani iliweka udhibiti wa sarafu ya dola mikononi mwa wenye benki binafsi ambao walipunguza urasimu wa makao makuu mjini Washington kwa kufungua matawi 12 katika majimbo mengine nchini Marekani.
Malengo ya awali
Benki hiyo ilitakiwa, bila kujali siasa, kuwa mamlaka ya mwisho ya ukopeshaji kwa mfumo wa benki pale yanapotokea mahitaji. Majukumu yake ya wakati huo na sasa yanaelezwa na mwenyekiti wa benki hiyo anayemaliza muda wake Ben Bernanke. "Malengo la awali la jaribio kubwa la kuanzishwa kwa benki kuu ya Marekani lilikuwa kulinda utulivu wa kifedha."
Sarafu hiyo ambayo ilikuwa ikipimwa kwa kiwango cha dhahabu iliyosafishwa, imekuwa sarafu ya dunia, na hadi sasa sarafu hiyo maarufu kama Green Buck, au Noti ya kijani bado inaendelea kuwa sarafu inayoongoza kwa matumizi duniani.
Kuanzishwa kwa benki hiyo kulifuatiwa na changamoto kadhaa katika miongo iliyofuata ambazo zinabainishwa mwenyekiti wake Bernanke: "Mdororo mkubwa wa kiuchumi wa miaka ya 1930, kupitia mfumuko mkubwa wa bei katika miaka ya 1970, hadi kwenye mgogoro wa kifedha wa mwaka 2008."
Yalaumiwa kwa kuchochea migogoro
Lakini wakosoaji wanasema maamuzi yasiyo sahihi ya benki hiyo yalichangia migogoro hiyo. Wanailaumu benki kwa kuingilia mambo yasiyoihusu, kwa mfamo kupitia sera yao. Mwenyekiti wa zamani wa benki hiyo Alan Greenspan, anatuhumiwa si tu kwa kuupuuza mfumuko wa hivi karibuni katika masoko ya nyumba, lakini pia aliuchochea kwa kutumia sera ya benki hiyo. Ni mfumuko huo ambao mwaka 2007 ulisababisha mgogoro mbaya zaidi wa kiuchumi tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia.
Wakosoaji wanasema mrithi wa Greenspans, Bernanke aliushughulikia mgogoro huo kwa pupa kwa kutumia sera ya fedha nafuu kupita kiasi, kama anavyosema James Dorn kutoka taasisi ya ushauri ya Cato ya mjini Washington. "Mtikisiko wa mwaka 2007 na mgogoro wa kifedha uliyofuatia vimesababisha sera ya fedha zenye masharti nafuu zaidi kupitia benki kuu."
Kwa muda mrefu, wakosoaji wanasema benki iliyaweka kapuni malengo ya kuanzishwa kwake, hasa ya kusimamia utulivu wa bei na kuhakikisha upatikanaji wa ajira. Kwa mantiki hii, benki hiyo imejiwekea malengo chini ya uongozi wa Bernanke, yakiwemo kuendeleza sera yake ya viwango vya chini kabisa vya riba ya karibu asilimia sifuri hadi hapo viwango vya ukosefu wa ajira vitakaposhuka kabisa.
Mwanamke wa kwanza kuchukuwa hatamu Januari
Lakini pia benki hiyo inakosolewa kwa sera yake ya ununuzi wa dhamana za muda mrefu za serikali na hati za dhamana za mali zisizohamishwa kila mwezi tangu kuanza kwa mgogoro wa kiuchumi mwaka 2007. Hii, anasema mchumi John Allison, ndiyo sababu ya uchumi wa dunia kuendelea kuwa dhaifu, na anapendekeza benki hiyo ifutuliwe mbali.
Wanasiasa kadhaa hasa wa mrengo wa kulia wanataka benki hiyo ifutwe, huku wengine wakisema ianze kupima ufanisi wake kwa malengo mapya. Wengine wanaonelea kuwa benki hiyo inapaswa kujikita katika kupambana na mfumuko wa bei na kuachana na sera ya soko la ajira. Mwenyekiti mpya Janet Yellen atachukuwa hatamu mwishoni mwa mwezi Januari, lakini wataalamu wanasema sera ya benki hiyo kuu haitabadilika sana chini ya uongozi wake.
Mwandishi: Passenheim Antje
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba