Mzozo wa kisiasa wadumu miaka 3 Burundi
15 Mei 2018Machafuko hayo yamezusha wasiwasi wa kutokea tena kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotokea mwaka 1993 hadi mwaka 2006 na kuwaua watu 300,000. Nchi hiyo inapoelekea kupiga kura ya maoni juu ya marekebisho ya katiba siku ya Alhamisi Mei 17, marekebisho ambayo yatamruhusu Nkurunziza kuendelea kuwa Rais wa nchi hiyo hadi mwaka 2034, hali hii ni kumbukumbu ya machafuko yaliyotokea miaka mitatu iliyopita.
Tarehe 26 mwezi Aprili mwaka 2015 siku moja baada ya Nkurunziza kutangazwa na chama chake cha CNDD-FDD kuwa mgombea wa urais kwa muhula wa tatu, maelfu ya raia wa Burundi waliandamana kupinga uamuzi huo wakisema kuwa ni ukiukwaji wa demokrasia. Mwanzoni mwa wiki sita za maandamano yaliyofanyika karibu kila siku, polisi walitumia nguvu kuyazuia ambapo watu kadhaa waliuwawa na wengine kuwekwa kizuizini.
Wapinzani wanasema kuwa mipango hiyo ya kumfanya Nkurunziza kubakia madarakani ni kinyume cha katiba na inakiuka mkataba wa amani ambao ulisaidia kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Nkurunziza mwenyewe anasema muhula wake wa kwanza wa urais wa mwaka 2005 hauhesabiki kwa sababu alichaguliwa na bunge na hakuchaguliwa moja kwa moja na wananchi.
Siku ya tarehe 13 mwezi Mei, jaribio la mapinduzi yaliyoongozwa na mkuu wa zamani wa jeshi la Burundi yalishindikana na kwa hatua hiyo, Nkurunziza alimfukuza kazi mlinzi wake pamoja na waziri wa mambo ya kigeni. Baadae mwezi june kiongozi wa bunge Pie Ntavyohanyuma alitangaza kwamba amekimbilia Ubelgiji, huko aliungana na idadi kubwa ya viongozi wa upinzani wa Burundi , waandishi wa habari, mashirika ya kiraia na wanachama wa chama tawala waliopo uhamishoni.
Siku ya tarehe 21 mwezi Julai Nkurunziza alichaguliwa tena kuwa Rais kwa muhula wa tatu kwa upigaji kura uliofanyika katika mvutano mkali.
Mfululizo wa matukio ya machafuko
Matukio ya utekaji yakafuatia. Mwezi wa nane mpambe wa karibu wa Nkurunziza Jenerali Adolphe Nshimirimana aliuwawa katika shambulizi la roketi. Siku moja baadae mtetezi wa haki za binadamu Pierre-Claver Mbonimpa alijeruhiwa na bunduki.
Mkuu wa zamani wa jeshi la Burundi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe , Colonel Jean Bikomagu, aliuwawa mwezi huo huo. Mwezi wa 12, watu takribani 87 waliuwawa katika mashambulizi ya kuratibu maeneo ya kijeshi ambayo husabaisha vitisho kwa vikosi vya usalama.
Miezi mitatu baadae, baraza la usalama la umoja wa mataifa iliidhinisha maafisa wa polisi 228 wa umoja wa mataifa nchini Burundi lakini serikali ya Burundi ikaukataa uamuzi huo.
Umoja wa mataifa ulitoa tathimini ya matukio hayo mwezi Septemba na kuishutumu serikali ya Burundi kwa kuhusika na matukio hayo ya uvunjwaji wa haki za binadamu.
Mwezi uliofuata serikali ya Burundi ikauambia umoja wa mataifa kuwa itajitoa katika mahakama ya kimataifa ya jinai ambayo imezindua uchunguzi wa awali wa madai ya mauaji, mateso na mambo mengine yanayokiuka haki za binadamu, na mwaka mmoja baadae Burundi ikajiondoa.
Mwezi Desemba Nkurunziza alitangaza atagombea tena urais mwaka 2020 Mwezi wa kwanza mwaka 2017 shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch liliwashutumu baadhi ya wananchama wa chama tawala
Mwezi wa nne tarehe 26, mwanaharakati aliyekuwa ametiwa kizuizini alihukumiwa kifungo cha miaka 32 gerezani kwa kushiriki maandamano ya mwaka 2015 yaliyokuwa yakimpinga Nkuruzinza kuwania muhula wa tatu. Tarehe 4 mwezi Mei vyombo vya habari vya kimataifa BBC na sauti ya America-VOA vilizuiliwa kurusha matangazo nchini Burundi kupitia Radio washirika.
Mwandishi: Veronica Natalis/ AFP
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman