Miaka 50 ya Uhuru wa Kenya
Tarehe 12 Disemba 1963, Kenya ilijitangazia uhuru wake. Hadi sasa, bado ukabila na mashambulizi ya kisiasa ni tatizo kubwa, lakini baada ya miaka hii 50, hapana shaka taifa hili linaweza pia kuangalia mafanikio yake.
Rais wa Kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta
Baada ya mapambano marefu ya ukombozi, hatimaye tarehe 12.12.1963, Kenya ilipata uhuru kutoka Uingereza. Mrithi wa Ufalme wa Uingereza Phillip (kushoto), Rais wa kwanza wa Kenya huru, Jomo Kenyatta, aliyetawala hadi kifo chake mwaka 1978. Wakati wa utawala wake aliweka jiwe la msingi la utukufu wa kabila lake la Kikuyu. Hadi sasa ukabila umekuwa tatizo kubwa kwa raia wa nchi hiyo.
Mlima Kenya jina la nchi
Baada ya ukoloni, nchi ilikuja kupewa jina la mlima wake mkubwa, Mlima Kenya, linatokana na neno la Kikuyu, Kere Nyaga, yaani mlima unaong'ara. Kwa watu wa eneo hilo, Mlima Kenya ni mahala patukufu ambapo mungu wao, Nagi, anaishi. Una urefu wa mita 5,000 na ni wa pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya Kilimanjaro. Volkano yake inakisiwa kuwa na umri wa miaka milioni tatu na nusu.
Mauaji ya Kisiasa
Kumetokea mauaji mengi ya kisiasa ambayo hakuna aliyewajibishwa kisheria: Gama Pinto (1964), Tom Mboya (pichani) waziri wa mipango na maendeleo ( 5.7.1969), Josiah Mwangi Kariuki - waziri chini ya utawala wa Jomo Kenyatta(2.3.1975 ); Waziri wa Mambo ya Nje wakati wa Moi, Robert Ouko, aliuawa tarehe 12.2.1990 baada ya kuanzisha uchunguzi wa shutuma za ufisadi dhidi ya tabaka la wanasiasa.
Utawala wa kidikteta wa miaka 24
Baada ya kifo cha Rais Jomo Kenyatta mwaka 1978, makamu wake, Daniel arap Moi, alichukuwa urais. Katika miaka yake 24 madarakani alijijenga kama mtawala katili. Wakosoaji walipotea na kufungwa jela. Ufisadi na uhalifu ulitawala na nchi ikawa dola ya kipolisi. Hali ya dharura ilivunja uhuru wa kisiasa. Moi alijikita madarakani kama watawala wengi madikteta wa Kiafrika kwa kujijenga mwenyewe.
Mashambulizi ya kwanza ya Al-Qaida barani Afrika
Mashambulizi dhidi ya ubalozi wa Marekani, Nairobi, tarehe 13.8.1998 yalipelekea vifo vya watu 247 na wengine 5,740 kujeruhiwa. Mara kwa mara kundi la al-Shabaab lenye uhusiano na al-Qaida limeishambulia Kenya, ikiwemo karibuni kwenye jengo la Westgate Nairobi, ambapo watu 67 waliuawa. Kenya ina wanajeshi wake kwenye Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM).
Matumaini yaliyopotea: Awamu wa Mwai Kibaki
Zaidi ya 60% mwaka 2002 walichamgua Mwai Kibaki wa Muungano NARC kuwa rais wa tatu wa Kenya huru, lakini hakutimiza ahadi zake za kupambana na ufisadi na kumteua Raila Odinga kuwa makamu wa rais. Baada ya uchaguzi uliozazaniwa mwaka 2007, Kibaki alijitangazia urais, na hivyo kupelekea machafuko yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000 na maelfu kadhaa kuwa wakimbizi wa ndani.
Ghasia baada ya Uchaguzi mwaka 2007
Baada ya uchaguzi wa Disemba 2007, mpinzani mkuu Raila Odinga alimtuhumu Rais Mwai Kibaki kuiba kura. Vyama na wanasiasa wakayahamasisha makabila kugombana. Mgogoro wa madaraka ukawa wa kikabila na kusababisha machafuko mabaya kuwahi kushuhudiwa nchini Kenya baada ya uhuru. Zaidi ya Wakenya 1,000 waliuawa na maelfu kujeruhiwa.
Demokrasia yapata Katiba Mpya
Rais Mwai Kibaki (kulia) akizindua katiba mpya tarehe 27.8.2010, inayoagiza mgawanyo wa madaraka, majimbo 47 mapya na bunge lenye mabaraza mawili kama vile la Marekani. Dhamira muhimu ya katiba hii mpya zilikuwa pia ni mageuzi ili kuondoa hali ya utawala wa kipolisi. Mageuzi ya mfumo wa mahakama yamekamilishwa, lakini Baraza la Usalama bado halijaanza. (AP Photo/Khalil Senosi)
Mahusiano mema na Ujerumani
Ujerumani ilikuwa ya kwanza kuitambua Kenya kwa mujibu wa sheria za kimataifa, mara baada ya nchi hiyo kupata uhuru. Kenya na Ujerumani zina mahusiano mazuri ya kiuchumi kwa muda mrefu. Watalii wengi wa Ujerumani hutembelea hifadhi za wanyama na mandhari za kuvutia za fukwe za Kenya. Kenya inaiuzia Ujerumani mbogamboga, maua, chai na kahawa. Kansela Angela Merkel alitembelea Kenya mwaka 2011.
Rais Mtuhumiwa
Uhuru Kenyatta, ambaye ni mtoto wa rais wa kwanza wa Kenya, na mgombea wake mwenza, William Ruto, walishinda kwa ushindi mwembamba wa asilimia 50.07 katika uchaguzi mkuu wa Machi 2013 wakisimama kwa niaba ya Muungano wa Jubilee. Uhuruto, kama wawili hawa wanavyojuilikana, wanakabiliwa na kesi mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinaadamu.
Wakimbiaji Bora Duniani
Kip Keino alishinda mashindano ya mbio za mita 1,500 mwaka 1968 kwenye mji mkuu wa Mexico na kuipatia Kenya medali ya kwanza ya dhahabu. Hapo ndipo jina la Wakenya lilipoanza kufahamika m kwenye mashindano ya mbio za kimataifa wakichuana na Waethiopia. Katika orodha ya mbio duniani, Wakenya wanashika nafasi nne za mwanzo: Wilson Kipsang, Patrick Makau Musyoki, Dennis Kimetto na Emmanuel Mutai.
Nishani ya Amani ya Nobel kwa "Mama Miti"
Katika miaka ya '90, akiwa profesa wa kwanza mwanamke Afrika ya Mashariki, Wangari Maathai aliyejulikana kama Mama Miti, alianzisha Vuguvugu la Ukanda wa Kijani ambalo lilipanda miti ipatayo milioni 40. Mara kadhaa alitiwa nguvuni na serikali. Kwa mchango wake kwenye maendeleo, amani na demokrasia, alitunukiwa Nishani ya Amani ya Nobel mwaka 2004. Alikufa tarehe 25.9.2011 akiwa na miaka 71.
Gazeti kongwe kuliko yote Kenya
The Standard lilianza kazi kama jarida la kila wiki, East African Standard, mwaka 1902. Tarehe 1.3.2006, polisi wazivamia ofisi za gazeti hilo na za televisheni ya KTN wakaharibu vifaa na kuchoma moto magazeti. Sababu ilikuwa ni taarifa ya Rais Mwai Kibaki kukutana kwa siri na kiongozi wa upinzani. Bibi wa kambo wa Rais Barack Obama, Sarah Obama, pia mara kwa mara husoma gazeti la The Standard.
Ukale na Usasa: Silicon Savannah
Sekta ya teknolojia ya habari na simu za mikononi inakuwa kwa haraka Kenya. Wakenya ni mashuhuri kwa ugunduzi wao katika matumizi ya simu za mikononi ama iwe ni kwa utumaji wa fedha kupitia M-Pesa, utengenezaji wa programu kwa ajili ya soko la bidhaa za kilimo au bima kupitia simu. Licha ya kuishi mbali na mji, hata jamii ya Kimaasai haitaki kuishi bila kutumia simu za mkononi.