1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miezi miwili ya vita vya mateso kwa raia wa Sudan

15 Juni 2023

Jeshi la Sudan limevishutumu Vikosi vya Msaada wa Dharura(RSF) kwa kumteka na kumuwa gavana wa jimbo la Darful Magharibi huku mapigano yakiendelea kuripotiwa katika maeneo tofauti ya taifa hilo.

https://p.dw.com/p/4SaEJ
Sudan Ärzte ohne Grenzen
Picha: ASHRAF SHAZLY/AFP

Ikiwa imetimia miezi mwili kamili tangu kuzuka kwa vita hiyo, kupitia ukurasa wake wa Facebook, jeshi limeandika "Mauwaji ya Khamis Abdullah Abakar yanamaanisha kwamba RSF imeongeza "sura mpya kwenye rekodi yake ya uhalifu wa kinyama ambayo imekuwa ikifanya dhidi ya watu wote wa Sudan," na kuliita tukio hilo kuwa "kitendo cha kikatili."

Jumanne iliyopita akizungumzia hali ya Darfur, mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker Perthes, alisema "kuna mtindo unaoibuka wa mashambulizi makubwa dhidi ya raia kwa msingi wa  utambulisho wao wa kikabila, unaodaiwa kufanywa na wanamgambo wa Kiarabu na baadhi ya watu wenye silaha, wakiwa katika sare za wapiganaji wa RSF.

Taarifa ya mashambulizi katika miji ya Sudan

Sudan | Kind
Mtoto wa Kisudan akiwa katika kambi ya wakimbiziPicha: imago images/ZUMA Press

Katika maeneo ya mapambano, ndege za kijeshi zilishambulia kwa mabomu mji wa El Obeid nchini Sudan. Kwa mujibu wa mashuhuda jana Jumatano, jeshi Sudan lilifanya mashambulizi ya anga kwa mara ya kwanza huko El Obeid mji mkuu wa jimbo la Kordofan Kaskazini, kilomita zipatazo 350 kusini mwa mji mkuu, ambao umezingirwa na wapiganaji wa RSF tangu kuanza vita.

Mkazi mmoja wa mjini Khartoum, Ahmed Taha anasema kwamba wale waliosalia nchini humo wakabliwa na ukata wa vyakula, maji na madawa. Anasema taifa zima kwa hivi sasa hakuna kilichosalia, nchi nzima imeharibiwa kila mahala ukitupa jicho utashuhudia mabaki ya mabomu, risasi. Kila eneo la Sudan ni eneo la majanga.

Shida ya chakula, madawa na huduma muhimu

Kauli inayofanana na hiyo inatolewa na mkazi mwingine, Soha Abdulrahman."Kusema kweli tunateseka sana na vita hivi vilivyodumu kwa miezi miwili, imepita miezi miwili tuko katika hali mbaya ambayo hakuna anayeifahamu isipokuwa Mwenyezi Mungu, katika ukanda wa Magharibi, Al Junaynah, Al. Fashir, Nyala. Mjini Khartoum tumezingirwa kabisa, hatuna chakula, hakuna dawa, hakuna chochote."

Tangu Aprili 15, jeshi la Sudan linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan na Vikosi vya Msaada wa Dharura vya kijeshi vinavyoongozwa na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo vilianza makabiliano kwenye mapigano ya mijini ambayo yameacha vitongoji vyote vya mji mkuu Khartoum kuharibika.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mtaifa lenye dhima ya uhamiaji IOM zaidi ya watu milioni 2.2 wameyakimbia makazi yao, wakiwemo zaidi ya milioni moja kwa Khartoum pekee. Miongoni mwa hao zaidi ya 528,000 wamekimbilia mataifa jirani kutafuta hifadhi.

Soma zaidi:Miji ya Darfur yashambuliwa huku vita vya Sudan vikisambaa

Juhudi za upatanishi za Marekani na Saudi Arabia zimekwama baada ya kushindwa hatua ya utekelezaji wa kusitishwa mapigano kwa mara kadhaa, kutokana na ukiukwaji wa wazi wa pande zote mbili. Kwa upande wao mashirika ya misaada ya kiutu yamekuwa katika jitihada za kutaftua kufunguliwa kwa njia salama za kibinadamu ili kuruhusu usaidizi pasipo mafanikio.

Chanzo: AFP