Miili kadhaa yagunduliwa kwenye mto India
13 Mei 2021Vyombo vya habari vya India vimeripoti kuwa tangu wimbi la pili la COVID-19 lilipozuka na kusababisha ongezeko la vifo nchini humo, gharama za kuchoma maiti zimepanda. Inaelezwa kuwa hali hiyo inaweza kuwa imechangia kwa familia masikini ama kuzitupa maiti kwenye mto au kuzizika. Miili mingi iliyokuwa imefunikwa kitambaa ilikutwa jana imezikwa kwenye mto katika maeneo mawili ya wilaya ya Unnao iliyoko jimboni Uttar Pradesh.
Baadhi ya watu hawachomi maiti
Mkuu wa Wilaya ya Unnao, Ravindra Kumar amesema moja ya maeneo ni sehemu kubwa ambako maiti zinachomwa na hapakuwa na uthibitisho kwamba miili hiyo ilikuwa ni ya wagonjwa wa COVID-19. ''Baadhi ya watu kwenye jimbo hilo hawachomi maiti, bali wanazika kwenye mchanga katika mto. Maiti kadhaa zimezikwa hivi karibuni na tunachunguza tukio hilo,'' alifafanua Kumar
Takriban miili 100 ilisombwa na maji katika kingo za Mto Ganges kwenye wilaya za karibu katika jimbo la Uttar Pradesh na Bihar, mapema wiki hii. Katika wimbi la sasa la maambukizi, India inarekodi takriban visa 350,000 na vifo 4,000 kwa siku.
Ama kwa upande mwingine majimbo mawili ya India yamesema yanapanga kuwapa wananchi wake dawa ya Ivermectin kuzuia kupata virusi vya corona, licha ya Shirika la Afya Duniani, WHO kuionya India kuhusu kuchukua hatua hiyo. Majimbo ya Goa na Uttarakhand yanachukua hatua hizo kutokana na hospitali kufurika wagonjwa walioko katika hali mbaya.
Wakati huo huo, Urusi imerekodi visa vya kwanza vya aina mpya ya kirusi cha COVID-19 kilichogundulika nchini India kwenye mkoa wa Ulyanovsk. Gazeti la Kommersant limeripoti leo kuwa visa 16 vimethibitishwa miongoni mwa wanafunzi wa Kihindi wanaosoma kwenye Chuo Kikuu cha Ulyanovsk, umbali wa kilomita 700 mashariki mwa Moscow.
Dilyar Khakimov, afisa wa shirika la Rospotrebnadzor linalofuatilia masuala ya afya, amesema wanafunzi hao wamewekwa katika karantini na chini ya uangalizi wa madaktari. Awali Naibu Waziri Mkuu wa Urusi, Tatiana Golikova, alisema nchi hiyo haijarekodi visa vyovyote vya aina ya kirusi cha India.
Ujerumani yarekodi zaidi ya visa 17,000
Nchini Ujerumani, taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch imerekodi visa vipya 17,419 vya virusi vya corona katika muda wa saa 24 zilizopita na vifo 278.
Australia kwa upande wake imefikia makubaliano ya kusambaza dozi milioni 25 za COVID-19 zinazotengenezwa na Moderna. Chini ya mpango huo serikali ya nchi hiyo ina matumaini kwamba watu wazima wote wa Australia watakuwa na uwezo wa kupata chanjo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Brazil nayo itasitisha kutengeneza chanjo ya COVID-19 ya Sinovac kwa sababu nchi hiyo itaishiwa malighafi ifikapo Ijumaa. Maafisa katika jimbo la Sao Paulo wamesema usafirishaji wa chanjo hizo unafanywa na kampuni ya usafiri ya China ambayo imezuiwa na mamlaka ya jimbo hilo.
(DPA, Reuters)