Misaada ya kiutu imeanza kuingia nchini Myanmar
12 Mei 2008Ingawa misaada ya kimataifa imeanza kumiminika nchini Myanmar,mashirika ya kimataifa yanasema,misaada hiyo imepaswa kuwasili tangu siku kumi zilizopita,kimbunga Nargis kilipopiga.Leo ndio ndege tatu za mizigo ziliwasili mji mkuu Yangon kutoka Ufaransa,zikiwa na tani 110 za chakula,mahema, dawa,pampu za maji na vifaa vya usafi kutoka kwa kundi la Madaktari wasio na Mipaka.Hata ndege ya kijeshi ya Marekani imepeleka mablanketi,vyandarua na maji.
Balozi wa Marekani nchini Thailand,Eric John amesema,mbali na misaada hiyo,ni muhimu pia kuwaruhusu wataalamu wa miradi ya misaada kuingia Myanmar ili wapate kuratibu misaada hiyo kwa maelfu ya watu wanaokabiliana na maafa ya kimbunga.Kwani viongozi wa kijeshi wa Myanmar wanaotawala kwa mabavu nchini humo tangu miaka 46 wanapinga kuwaruhusu wataalamu wa kigeni na wanachelewesha kuwapatia viza wataalamu hao.
Myanmar ikiendelea kushinikizwa kubadili msimamo wake,wajumbe wa Umoja wa Mataifa pia wamekutana na majemadari waandamizi wa nchi hiyo katika juhudi ya kuwashawishi kuharakisha kuwapatia viza wataalamu wa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada.Kwani misaada ya kigeni hivi sasa inawasili mji mkuu Yangon ambao pia umeathirika,lakini ni eneo la Irrawaddy kwenye mdomo wa mto ndio lililoathirika vibaya zaidi na hadi hivi sasa ni wakaazi wachache mno waliopokea msaada.Katika eneo hilo,njia pekee ya usafiri ni mashua.
Tatizo jingine ni hatari ya kuzuka magonjwa kama vile kipindupindu na tumbo la kuhara huku mvua mpya zikitazamiwa kunyesha katika eneo la kusini lililoathirika vibaya zaidi.Wakati huo huo,shirika la WFP la Umoja wa Mataifa linatathmini kuwa limeweza kuwasaidia hadi watu 30,000 kwa kuwapatia chakula cha majuma mawili.Lakini kuna kama watu milioni 1.2 hadi milioni 1.9 walioathirika kwa kimbunga Nargis. Inakadiriwa kuwa hadi watu 100,000 wamepoteza maisha yao na wengine wapatao kama 220,000 bado hawajulikani walipo.
Hiyo kesho Kamishna wa Maendeleo na Misaada ya Kiutu wa Umoja wa Ulaya,Louis Michel atakutana na mawaziri wenzake wa umoja huo mjini Brussels na baadae ataelekea Myanmar.Anasema jumuiya ya kimataifa inapaswa kujitahidi zaidi kuokoa maisha ya watu wanaongojea kusaidiwa.