Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen ziarani Hodeida
23 Novemba 2018Martin Griffiths, aliyewasili katika mji mkuu wa Sanaa unaodhibitiwa na waasi tangu jumatano iliyopita, anajaribu kuzitanabahisha pande zinazohusika zishiriki katika mazungumzo ya Stockholm na kwa namna hiyo kumaliza miaka kadhaa ya vita vilivyoitumbukiza Yemen katika janga la njaa.
Mwanadiplomasia huyo wa Uingereza ameshawasili katika mji wa bandari unaozongwa na mapigano wa Hodeida. Ziara yake imelengwa kuwasihi waasi wa Houthi wanaoelemea upande wa Iran na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia wajizuwie mnamo wakati huu ambapo mazungumzo ya amani yanapangwa kuitishwa.
Maefu ya watoto wanakabiliwa na hatari ya kufa kwa njaa
Mzozo wa Yemen uliozidi makali baada ya ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia kuingilia kati mwaka 2015 umeshaangamiza maisha ya maelfu ya watu na kuwatumbukiza wayemen milioni 14 katika janga la kufa kwa njaa. Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia watoto -Save the Children, watoto 85 000 wa Yemen huenda wamekufa kwa njaa tangu mwaka 2015.
Katika mazungumzo yake jana pamoja na mkuu wa waasi wa Houthi, Abdel Malik al Houthi, mjumbe huyo maalum wa Umoja wa mataifa alizungumzia "njia zinazoweza kusaidia kuitisha mazungumzo ziada" pamoja na mapendekezo yaliyotolewa na Umoja wa mataifa ya kutaka zifunguliwe njia za kuwasafirisha majeruhi na wagonjwa wakapatiwe matibabu nchi za nje pamoja na kupata hakikisho wataruhusiwa kurejea nchini Yemen.
Kiongozi wa Houthi adai apatiwe hakikisho kutoka kwa mahasimu wao
Kwa mujibu wa msemaji wa waasi, kiongozi wa Houthi amemtaka kwa upande wake ahakikishe ahadi zitakazotolewa na mahasimu wao ni za "kuaminika na zitaheshimiwa."
Martin Griffiths aliliambia baraza la usalama la umoja wa mataifa wiki iliyopita pande zinazohasimiana nchini Yemen zimemhakikishia utayarifu wao wa kushiriki kwa dhati katika mazungumzo ya amani yatakayofanyika mwishoni mwa mwaka huu mjini Stockholm Sweden.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu