Mkanganyiko wazidi Syria
15 Juni 2012Wakati mauaji yakiendelea kuripotiwa nchini Syria, Urusi imekana kuhusika kwa namna yoyote kujadili na mataifa mengine juu ya mabadiliko ya uongozi wa juu nchini Syria.
Waziri wa Mambo ya Nje, Sergei Lavrov, amesema hayo muda mfupi uliopita na kusisitiza kwamba Urusi haina mpango wowote wa kuchangia katika kumuondoa Rais Bashar al- Assad madarakani.
Usiku wa kuamkia leo, jeshi la Syria limeyashambulia maeneo ya vijijini ya mji mkuu Damascus na katika eneo la kati ya nchi hiyo, ikiwa ni miezi 16 tangu vuguvugu la kuipinga serikali lianze.
Wanaharakati wa upinzani wameshuhudia miripuko ya mabomu,na ufyetuaji wa risasi usiku kucha wakati vikosi vya Rais Bashar -al- Assad na vya waasi vilipopambana.
Haytham al-Abdullah afafanua kadhia hiyo
Kwa mujibu wa mwanaharakati mmoja wa eneo hilo, Haytham al- Abdullah, askari hao waliuzingira mji wa Haouriyeh, uliopo karibu na Damascus na kuua watu tisa.
Akithibitisha taarifa hizo, mkuu wa Shirika la Haki za Binadamu la Syria, lenye makao yake makuu nchini Uingereza, Rami Abdel Rahman, amesema mpaka sasa bado haijulikani ni nani hasa aliyefanya mauaji hayo.
Aidha, Baraza la Upinzani la Taifa limesema watu hao tisa walikuwa ni wakulima na maiti zao zimekutwa bila mikono, miguu wala sehemu za siri.
Baraza hilo limesema jumla ya watu 84 wameuwawa jana pekee, na 48 kati yao ni raia. Kutokana na umwagaji huo wa damu, baraza hilo limeziomba nchi za kiarabu na kiislam pamoja na Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka na kukomesha mauaji hayo mara moja.
"Gaidi Mohammed Hussam al-Sadaki awekwa chini ya ulinzi"
Wakati huohuo, Shirika la Habari la taifa SANA limeripoti kukamatwa kwa "gaidi Mohammed Hussam al- Sadaki wa mtandao wa kigaidi duniani al- Qaeda". Sadaki anashukiwa kwa kutaka kujitoa mhanga ndani ya msikiti mmoja katika sala za Ijumaa, ya leo. Kutiwa nguvuni kwake kunatukia siku moja baada ya mlipuko wa bomu kutokea mjini Damascus na kujeruhi watu 14.
Gaidi huyo amekiri kuwepo kwa watu wengine walionuia kujitoa mhanga katika misikiti kadhaa katika mji mkuu huo.
Mara kadhaa utawala wa Rais Bashar -al-Assad umelaani makundi ya magaidi yenye silaha yanayoleta machafuko nchini Syria tangu katikati ya mwezi Machi, mwaka jana.
Mkutano wa Istanbul utazaa matunda?
Kwa upande mwingine, kambi ya upinzani inakutana mjini Istanbul, Uturuki kujadili namna ya kumaliza ghasia za nchini Syria.
Urusi nayo imekana tuhuma za Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, kwamba inatuma helikopta za kivita nchini Syria. Waziri wake wa Mambo ya Nje, Sergei Lavrov, amesema inachokifanya ni kutekeleza mikataba iliyopo ya kuipatia Syria vifaa vya ulinzi wa anga, ambavyo ni kwa ajili ya kujilinda na mashambulizi kutoka nje na si kwa ajili ya machafuko ya ndani ya Syria.
Mwandishi: Pendo Paul Ndovie
Mhariri: Saumu Mwasimba