1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkanyagano mkubwa watokea wakati wa mazishi ya Soleimani

Sylvia Mwehozi
7 Januari 2020

Kituo cha televisheni cha serikali ya Iran kimeripoti kuwa watu 35 wamepoteza maisha katika mkanyagano huo katika mazishi ya jenerali wa kijeshi aliyeuawa na Marekani katika mji wa Kerman.

https://p.dw.com/p/3VpWJ
Iran Trauer um General Soleimani in Kerman
Picha: Getty Images/AFP/A. Kenare

Hadi sasa imethibitika kuwa watu 35 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 48 kujeruhiwa kwenye mkanyagano huo, huku picha za televisheni zimeonesha vurugu ikitokea wakati harakati za mazishi zikiendelea. Ripoti kutoka wafanyakazi wa huduma za uokozi zinasema wapo watu waliopoteza maisha.

Mamilioni ya waombelezaji walianza kukusanyika katika mitaa ya mji huo wa kusini mashariki mwa Iran tangu alfajiri kwa ajili ya ibada ya mwisho ya mazishi ya kamanda huyo aliyeuawa wiki iliyopita katika shambulizi la anga la Marekani.

Mabaki ya mwili wa Soleimani na msaidizi wake Hossein Pourjafari ambaye aliuawa pia katika shambulio hilo, yaliwasili uwanja wa ndege wa Kerman na kufuatiwa na maandamano makubwa ya mazishi kwenye miji ya Iraq na ile ya Iran. Ibada ya mazishi ilifanyika katika viwanja vya wazi kabla ya jeneza lake kubebwa katika gari na kupitishwa mitaa ya Kerman. Waombolezaji wamesema kuwa wamefika hapo kutoa heshima zao za mwisho kwa kamanda wao aliyekuwa alama ya ulinzi.

Iran Trauer um General Soleimani in Kerman
Umati wa waombolezaji mjini KermanPicha: Getty Images/AFP/A. Kenare

Mkuu wa jeshi la wanamapinduzi la Iran ametoa kitisho kwamba "watayachoma moto" maeneo yanayosaidiwa na Marekani. Hossein Salami ametoa kauli hiyo mbele ya umati wa maelfu ya watu waliokusanyika mjini Kerman.

"Tunarudia tena kwamba! nia yetu ni madhubuti. Tunawaambia adui zetu kwamba tutajibu lakini kama watachukua hatua nyingine, tutachoma moto maeneo wanayoyapenda na kuthamini" alisema kiongozi huyo.

Matamshi yake yanalingana na yale yaliyotolewa na maafisa wa juu wa Iran kuanzia kiongozi wa juu Ayatollah Ali Khamenei na viongozi wengine. Siku ya Jumatatu rais wa Iran Hassan Rouhan alimuonya Trump "kamwe kutoitisha Iran" baada ya kiongozi huyo wa Marekani kutoa orodha ya maeneo 52 ambayo wanaweza kuyashambulia ndani ya Iran. Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammed Javad Zarif amesema Marekani imekataa kumpatia visa kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini New York.

Zarif ametoa kauli hiyo wakati nchi yake ikijiandaa kumzika kamanda Soleimani, na kusema kwamba "wana hofu mtu atakwenda Marekani na kusema ukweli". Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani haijatoa kauli yoyote juu ya kukataliwa visa ya Zarif, ingawa kama mwenyeji wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa inapaswa kutoa vibali kwa maafisa wa kigeni kuhudhuria mkiutano kama hiyo.